Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
KILIMO cha kahawa wilayani Monduli, mkoani Arusha, kimeanza kuwekewa mikakati itakayowawezesha wakulima kurejesha imani ya kuendelea kulima zao hilo la kibiashara.
Kuzorota kwa kilimo cha zao hilo wilayani hapa kulichangiwa na mambo mengi, ikiwamo kukosekana kwa bei nzuri katika soko.
Hayo yalibainishwa wilayani hapa juzi na Mkuu wa Wilaya hiyo, Idd Kimanta, kwenye mkutano mkuu wa Chama cha Wakulima wa Kahawa wilayani hapa.
Akizungumza na wadau hao wa kahawa, Kimanta alisema, wakulima hawana sababu ya kukata tamaa ya kuendelea kulima zao hilo, badala yake wazingatie ulimaji bora, kwani bei ya zao hilo bado ni nzuri sokoni.
“Mkakati uliopo ni kuhakikisha zao hili linafufuliwa kwa juhudi zote na kuifanya wilayani yetu kuwa miongoni mwa wilaya zinazozalisha kahawa yenye ubora nchini,” alisema Kimanta.
Alisema ili kuinua kilimo, DC Kimanta aliwataka wakulima hao kujipanga kushirikiana na maofisa ugani ili waweze kuwatembelea na kuwapa ushauri wa kitaalamu.
“Sitaki kuona zao hili likififia wilayani kwangu. Binafsi nasikitika kuona zao la kahawa likiwa halipewi kipaumbele. Katika jitihada hizi Halmashauri mnatakiwa kuwa na kitalu cha miche ya kahawa na dawa za kuulia wadudu ili kuwezesha wakulima kupata mbegu bora za kisasa zitakazoweza kuwa na matokeo yenye tija,” alisema.
Alisema wilaya hiyo ina jumla ya mashamba ya kahawa yenye ekari 127, huku maeneo ya vijiji vya Orarash, Ngarash Mlimani na Engutoto yakifaa zaidi kwa kilimo hicho.
Akifafanua kuhusu uzalishaji, alisema umekuwa ukipanda na kushuka, ambapo mwaka 2012 zilizalishwa tani 12, mwaka 2013 tani 12, mwaka 2014 tani 42, mwaka 2015 tani 18 na mwaka 2016 zilizalishwa tani 25.
Kwa upande wake, Mratibu wa zao la Kahawa Mkoa wa Arusha, Anascola Sanda, alisema ili wakulima hao wavune mazao bora wana kila sababu ya kutumia mbegu za kisasa zenye uwezo wa kuzaa zaidi.
“Ili kuongeza mavuno lazima wakulima wapande miche mipya ya kisasa, ambapo mche mmoja hutoa kilo tatu za kahawa kwa mkupuo mmoja na utaendelea kuzalisha kahawa kwa mikupuo mingine.
“Niwahakikishie kwamba mfuko wa zao la kahawa utawaletea mbegu bora, hivyo ni muhimu mkalima kwa kuzingatia kanuni 10 za uzalishaji wa kilimo,” alisema.