LONDON, UINGEREZA
WATU saba wameuawa na wengine zaidi ya 30 wanatibiwa hospitali baada ya watu wanaoaminika kuwa magaidi kuendesha gari na kuwagonga wapita njia kisha kuwachoma visu watu waliokuwa baa usiku wa kuamkia jana.
Washambuliaji watatu ambao walikuwa wamevalia mikanda ya bandia ya milipuko, pia walipigwa risasi na polisi na kufa. Polisi mjini hapa wamesema.
"Katika wakati huu, tunaamini watu saba wameuawa pamoja na washambuliaji watatu waliopigwa risasi na polisi," alisema Kamishna Msaidizi wa Polisi Mark Rowley ambae pia ni mkuu wa kitengo cha kupambana na ugaidi.
Washukiwa waliwagonga wapita njia katika daraja la London kabla ya kuwashambulia watu waliokuwa baa za karibu na migahawa, Rowley alisema.
Polisi wenye silaha waliwapiga risasi washambuliaji watatu katika muda wa dakika nane baada ya kupokea simu ya kwanza kuhusu mashambulio.
Watu walioshuhudia waliliambia gazeti la Guardian kuwa waliwaona watu wawili wakiwachoma visu watu nje ya mgahawa maarufu wa Roast katika Soko la Borough.
“Walikuwa wakiwachoma visu watu, tulikuwa tunapiga kelele ‘acha, acha’ na watu walikuwa wakiwatupia viti kabla ya polisi kuwasili na kuwapiga risasi,” shuhuda mmoja alisema.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ameliita shambulio hilo kuwa ‘tukio la kigaidi’ na alieleza ‘shukrani zake nyingi’ kwa polisi na huduma za dharura.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amempigia simu May na kumpa rambi rambi zake kufuatia tukio hilo.
Aidha viongozi mbalimbali duniani akiwamo Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Kiongozi wa Ujerumani, Angela Merkel wamelaani vikali tukio hilo.
Shambulio hilo ambalo limetokea ikiwa ni wiki kadhaa tu baada ya watu 22 kuuawa baada ya mtu mmoja wa kujitoa mhanga kujilipua ndani ya ukumbi wa burudani mjini Manchester.