24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DK. TIZEBA ATAKA WASINDIKAJI MAZIWA WAWEZESHWE

Na MWANDISHI WETU-BUKOBA


WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, ameiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB),  kuharakisha kutoa mikopo kwa wasindikaji wa maziwa ili kuongeza tija kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini.

Waziri Dk. Tizeba alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa Benki hiyo katika Kilele cha Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki ya Maziwa, iliyokuwa ikifanyika Kitaifa mjini Bukoba, mkoani Kagera.

Alisema utoaji wa mikopo kwa wasindikaji kuna umuhimu wa kipekee, kwa kuwa utachangia uhakika wa masoko kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini, hali itakayochochea tija kwa wafugaji hao, hivyo kuchagiza lengo la Serikali la Awamu ya tano ya kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuweza kunufaika na sekta hizo.

“Serikali imedhamiria kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi, hivyo uanzishwaji wa Benki ya Kilimo lazima kusaidie katika kuhakikisha wasindikaji wa maziwa wanapata huduma za TADB kwa wakati, ili tupate uhakika wa masoko kwa wafugaji wetu ili tuiinue tasnia ya maziwa ichangie ukuaji wa uchumi na maendeleo nchini,” alisema.

Kwa mujibu wa mpango kazi wa TADB, sekta ya mifugo ni mojawapo ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali, hasa katika uongezaji wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa nchini.

Kutokana na hali hiyo, TADB imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa, ili kuongeza tija kwenye tasnia za nyama na maziwa na kuchagiza maendeleo katika tasnia hizo.

TADB ni taasisi ya serikali ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha za mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini, ambao ulikuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa, riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles