Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA
WAKULIMA zaidi ya 70 wa mpakani mwa Kongwa mkoani Dodoma na Kiteto mkoani Manyara, wamefanya maandamano ya amani kwa lengo la kuonana na Waziri Mku, Kassim Majaliwa, wamueleze kilio chao cha kuporwa maeneo yao ya kilimo.
Wakulima hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nalau kijiji cha Kiteto Kata ya Lenjulu, Daimon Chimulu, walisema wamelazimika kufanya maandamano kutoka wilayani Kongwa hadi Dodoma kuonana na Waziri mkuu kumueleza kero zao za kuporwa mashamba yao ya Lumilumi na kutaka maeneo hayo yatumiwe na wafugaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti huyo alisema pamoja na kufanya maandamano kwa ajili ya kuonana na Waziri Mkuu aweze kutatua mgogoro walionao, juhudi zao za kuonana naye zimegonga mwamba kutokana na kutokuwapo ofisini kwake.
Mwenyekiti huyo alisema kilio chao ni kutaka kupewa mashamba yao waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo kwa vile kwa sasa hawajui hatma ya maisha yao ingawa wapo katika maeneo hayo kwa muda mrefu.
“Sisi wakulima wa eneo la Lumilumi tunahitaji kujua hatma yetu kwa sababu tumezuiliwa kufanya shughuli zetu za uzalishaji kwa maana ya kilimo na tumeambiwa tusifanye shughuli yoyote ya kilimo wala wafugaji wasiingize mifugo katika maeneo hayo.
“Jambo la kushangaza kwa sasa tumekuwa tukiona mifugo ikiingia katika maeneo yetu na kula mazao yetu jambo ambalo lisasababisha kuwapo viashiria vya machafuko au kutoweka amani kutokana na mgogoro huo.
“Imefikia hatua ya wafugaji kuanza kuwashambulia wakulima kwa fimbo huku hakuna hatua yoyote ya sheria ikichukuliwa,” alisema Mwenyekiti huyo.