31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri agoma kuzindua umeme wa Rea

NA HADIJA OMARY -LINDI

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amekataa kuwasha umeme   kwenye mradi wa  Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika vijiji vya Nangambi na Kisandi  wilayani  Kilwa Mkoa wa Lindi baada ya kutoridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo.

Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo, Mgalu alieleza sababu ya kukataa  kuwasha umeme huo kuwa ni udogo wa kasi ya utendaji wa kazi.

Mgalu alisema hali hiyo ilisababisha uchache wa wananchi waliofikishiwa umeme na kutokamilisha miundombinu ya umeme katika maeneo hayo.

Alisema Serikali inatafakari kama ni busara kuendelea na wakandarasi wanaozembea na kuchelewesha malengo ya kupeleka umeme kwa wananchi vijijini.

Hata hivyo, licha ya  kukataa kuwasha umeme huo, Mgalu alimpa mkandarasi wiki moja kuhakikisha anamalizia kuweka miundombinu katika vijiji hivyo  wananchi waanze kupata huduma.

  Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa, Haji Mbaruku, alisema katika mradi huo wa REA  awamu ya tatu    kata 10 na vijiji 25 vinatarajiwa kufikiwa.

  Alisema kata hiyo ya Mingumbi ndiyo itakayonufaika zaidi na mradi huo kwa vile  ina vijiji sita vitakavyopitiwa na mradi huo.

Alisema Wilaya ya Kilwa ina  vijiji 90 na mpaka sasa ni vijiji 34 ndivyo vilivyounganishiwa umeme.

Naibu waziri alisema kuunganishwa kwa vijiji vingine 25 ambayo vipo katika mradi wa REA awamu ya tatu, kutafanya kufikia vijiji 59 vinavyopata huduma hiyo.

  Meneja wa Tanesco Wilaya ya Kilwa, Rajabu Haule, alisema katika kitongoji cha Nangambi mkandarasi alitakiwa kujenga transifoma moja ambayo tayari  imeshawekwa.

Alisema pia anatakiwa kujenga njia ya umeme LV line na service line kwa kilomita mbili na mpaka sasa mkandarasi huyo amejenga kilomita 0.35 au asilimia 17 za utekelezaji.

“Katika kitongoji hiki tulikusudia wateja 33 ambako kati ya hao wateja 30 walikuwa ni wa njia moja na wateja watatu walikuwa ni wa njia tatu lakini mpaka sasa ni wateja saba  tu ndiyo waliofikiwa na umeme,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles