28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kufanyia marekebisho Sheria Kanuni ya Adhabu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Sheria ya Kanuni ya Adhabu inahitaji marekebisho makubwa kwa kuwa tangu ilipopatikana haijafanyiwa mabadiliko yoyote.

Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Novemba 25,2024 wakati akizindua kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Amesema sura ya 16 ya sheria hiyo imeeleza kwa kina kuhusu ukatili wa kijinsia lakini kuna maeneo ya kufanyia kazi na kuboresha zaidi ili kuweza kushughulikia ipasavyo masuala ya ukatili wa kijinsia.

“Ukatili wa kijinsia ni suala la aibu linalobeza kundi kubwa katika jamii hasa wanawake na watoto, si suala la fahari au la kulitetea, ni suala la kusema hili jambo ni baya na kulichukulia hatua.

“Tuna sheria nzuri zinazoshughulikia masuala ya ukatili na kijinsia kama Sheria ya Kanuni ya Adhabu, lakini inahitaji marekebisho tangu ilipopatikana haijafanyiwa mabadiliko kwahiyo inahitaji mabadiliko makubwa,” amesema Profesa Kabudi.

Aidha amesema licha ya Tanzania kupiga hatua katika mapambano hayo bado inahitaji kupiga hatua zaidi na kutaka kila mmoja awe balozi wa kupinga ukatili wa kijinsia.

Naye Mwenyekiti wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Dk. Monica Muhoja, ameiomba Serikali kutunga sheria mahususi ya kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia ili kupunguza vitendo hivyo.

Amesema wanawake na watoto wameendelea kuwa waathirika wa vitendo hivyo na kwamba wako tayari kubainisha mapungufu yaliyopo kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu kwa kuwa walifanya utafiti.

Kwa upande wake Mratibu wa Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (Mkuki) ambaye pia ni Mkurugenzi wa WiLDAF, Wakili Anna Kulaya, amewahamasisha wananchi kuchagua viongozi bora ambao hawatavumilia ukatili wa kijinsia.

“Ukatili wa kijinsia ni janga la taifa hasa ubakaji na ulawiti ambapo waathirika wakubwa ni wasichana na watoto, tunahitaji uwajibikaji wa kila mtu katika kushughulikia ukatili wa kijinsia,” amesema Kulaya.

Balozi Dk. Getrude Mongela ambaye alikuwa mgeni wa heshima katika hafla hiyo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wanapaswa kuweka mkakati wa kumalizia kazi iliyobaki baada ya mkutano wa Beijing uliofanyika mwaka 1995.

Amesema mkutano huo uliainisha maeneo 12 ya kufanyiwa kazi na licha ya kupiga hatua kama nchi lakini bado kuna kazi ya kufanya ili kuwa na dunia yenye amani na ambayo binadamu wote ni sawa.

Siku 16 za uanaharakati dhidi ya ukatili wa kijinsia ni mbinu inayotumiwa na Mkuki ili kuifikia jamii kubadili fikra na mitazamo inayochochea ukatili wa kijinsia.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema “Kuelekea miaka 30 ya Beijing; chagua kutokomeza ukatili wa kijinsia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles