NA GUSTAPHU HAULE
-PWANI
Ukosefu wa magari ya wagonjwa (Ambulance) katika Kata ya Kibindu, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze umesababisha wajawazito kupanda magari ya mkaa kufuata huduma ya uzazi katika vituo vya afya vilivyopo nje ya kata hiyo.
Diwani wa Kata hiyo Ramadhani Mkufya(CCM) amebua hoja hiyo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika jana Mjini Lugoba, ambapo amesema wajawazito na wagonjwa wengine katika kata yake wamekuwa wakikabiliwa na adha hiyo kwa muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo Mkufya ameiomba Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake Edes Lukoa kuhakikisha inapeleka gari la wagonjwa katika Kata hiyo ili kuweza kuokoa maisha ya wananchi wake hususani wajawazito.
“Kama halmashauri haina uwezo wa kununua magari mapya ni vyema kwa sasa wakaweka jitihada za kutengeneza magari mabovu yaliyopo ili yawasaidie wananchi hao wakati taratibu za kununua magari mapya zikiendelea kufanyika,” amesema Mkufya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Edes Lukoa, amesema kilio cha diwani huyo ni sahihi na kwamba halmashauri itatumia mapato yake ya ndani katika kumaliza tatizo hilo.
Hata hivyo, amesema halmashauri inatengeneza ambulance moja mbovu iliyokuwa ikifanya kazi katika maeneo ya Kwa Mrohombo na kwamba inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na itapelekwa katika kata.