31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

TUONANE MAHAKAMANI, RAILA AMWAMBIA UHURU

NAIROBI, KENYA

KIONGOZI wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, jana ametangaza kuwa wanahamia Mahakama ya Juu kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8, mwaka huu.

Awali NASA ilisema kuwa safari hii haitakuwa na mpango wa kwenda mahakamani kwa kile ilichokiita mfumo wa mahakama umetishwa na Serikali na hivyo hauwezi kutoa hukumu ya haki.

Akizungumza katika ofisi za Okoa Kenya jijini hapa jana, Raila alisema ushindi wa Uhuru uliotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ijumaa iliyopita ni wa ‘kutengenezwa na kompyuta’.

Alisema uamuzi wa kumkabili Uhuru mahakamani kwa kiasi fulani unachochewa na fungia fungia inayoendelea dhidi ya mashirika yanayounga mkono demokrasia.

Serikali ilitangaza kuyafuta mashirika ya demokrasia na haki za binadamu, ikiwamo Tume ya Haki za Binadamu Kenya (KHRC) na Kituo cha Utawala Bora Afrika (AfriCOG), ambayo yamekuwa yakiukosoa utawala wa Jubilee.

Kuna minong’ono pia kuwa mashirika hayo yalikuwa yakijiandaa kwenda mahakamani kupinga ushindi wa Uhuru.

Hata hivyo, kufuatia kelele zilizopigwa na Umoja wa Mataifa (UN), Transparent International na mashirika mengine ya haki za binadamu, Serikali ya Kenya jana ilitangaza kusitisha hatua ya kuyafutia usajili mashirika hayo inayoyatuhumu kukwepa kodi na kuajiri wageni kinyume cha sheria.

Raila alisema lengo lao kuu mahakamani ni kuionyesha dunia namna rais anavyotengenezwa kwa kompyuta.

“Tutaionyesha dunia namna takwimu zilivyopikwa na Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi,” alisema Raila akiwa ameambatana na vinara wenzake wa NASA; Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi.

“Wakenya hawatakubali kuongozwa na viongozi wanaotokana na kompyuta,” aliongeza.

Alisema matokeo yaliyotangazwa na IEBC hayakutokana na fomu 34B, nyaraka ambazo zilisainiwa na mawakala wa vyama na wagombea katika majimbo ya uchaguzi.

“Jana (Juzi) Chiloba alikiri fomu zote 34B hazikuwepo na hivyo, matokeo hayakuwa halali,” alisema, akimrejea Mtendaji Mkuu wa IEBC, Ezra Chiloba.

Kauli yake ilikuja saa chache baada ya tume kutuma ujumbe katika akaunti yake ya Twitter, kwamba fomu zote 34B kutoka majimbo yote ya uchaguzi zinapatikana kwa umma kuzipitia.

“Uamuzi wetu wa kwenda mahakamani unatoa fursa ya pili kwa Mahakama ya Juu. Mahakama inaweza kutumia fursa hii kujisahihisha au kama 2013 inaweza kuzidisha matatizo kwa nchi hii.

“Zaidi ya hayo, tunachukua hatua hii kwa niaba ya wale waliozuiwa kwenda mahakamani. Serikali imeanzisha vita ya kufungia mashirika ya kiraia yaliyokuwa yakijaribu kwenda mahakamani. NASA inataka kuionesha dunia uchafu huu.

“Wakati tukienda mahakamani, tunatambua kwamba tangu Uhuru Kenyatta na William Ruto waionye mahakama hadharani, IEBC haikupoteza hata kesi moja mahakamani.

“Kwa kwenda mahakamani hatuhalalishi miito ya baadhi ya waangalizi kututaka tukubali matokeo, bali ni kwa ajili ya wale waliojitoa mhanga kusimama mistari mirefu Jumanne ya Agosti 8, 2017, kina mama na watoto wao wakiwa mgongoni, wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee kwa vijana waweze kusikika,” alisema Raila.

NASA ina hadi kesho kufungua kesi Mahakama ya Juu, ambayo itakuwa na siku 14 za kusikiliza na kutoa uamuzi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles