Na FERDNANDA MBAMILA, DAR ES SALAAM
TAASISI isiyo ya kiserikali inayojihusisha na usindikaji wa vyakula mbalimbali nchini ya Tanzania Food Processing Association (Tafopa), imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo ili kufikia lengo wanalotarajia.
Lengo la Taasisi hii ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo ili kuwakomboa katika suala zima la utengenezaji wa bidhaa mbalimbali katika mazingira yaliyo salama.
Pia taasisi hiyo imeiomba Serikali iwasaidia kwa kuwatengea maeneo maalumu ya viwanda ambayo yatakuwa yamesheheni huduma zote za kijamii na zinazohitajika katika viwanda hususani umeme na maji.
Hii inatokana na kuwepo kwa wajasiriamali walio wengi kuwa na taaluma ya elimu ya kutosha juu ya usindikaji wa bidhaa, lakini kinachowakwamisha na kushindwa kuendelea ni kukosa wadau wa kuwawezesha ili kufikia malengo waliyoyakusudia.
Moja kati ya changamoto inayowakumba wajasiriamali hao ni kukosa vifaa vya kusindikia bidhaa hizo ambapo wangeweza kupata wadau watakaoweza kuwasaidia kwa wakati na hivyo wangefika mahali sahihi katika suala zima la usindikaji wa vyakula.
Lakini changamoto hiyo imegeuka kuwa chungu zaidi baina yao kwa kuendelea kufanya kazi katika mazingira hafifu ambapo kama msindikaji unatakiwa kuwa na sehemu maalumu kwa ajili ya kufanyia shughuli hizo na si katika makazi ya kuishi.
Ingawa Tanzania ya sasa imeanza kuwa na uwepo mwingi wa viwanda mbalimbali vya uchakataji na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, lakini hakuna mipango thabiti kwao ya kuwasaidia katika zoezi zima.
Mwenyekiti wa Chama cha Usindikaji wa vyakula nchini, Suzy Laiza, anasema wao kama Taasisi ya Mayoda wamewawezesha wasindikaji wadogo ili waweze kupata maeneo maalumu ya usindikaji wa bidhaa hizo.
Anasema hadi sasa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (Sido), wameweza kutuunga mkono kwa kuwapa mafunzo ya usindikaji wa vyakula kwa wajasiriamali wadogo zaidi 600 katika taasisi hiyo ili kuwasaidia wajasiriamali hao kufikia malengo yao.
“Hapo awali wasindikaji walikuwa wanafanya shughuli zao wakiwa katika majumba yao kwa kukosa sehemu maalumu ya kuzalisha bidhaa hizo, kwani kama wana ujuzi na maarifa ya kutosha na uwezo wa kuweza kuzalisha na wameonyesha moyo kwanini wasisaidiwe!”anasema Laiza.
Tuliona ni vyema zaidi kwa kupitia mkutano tulioufanya Novemba 13, mwaka jana wa kuwakutanisha wadau wa sekta mbalimbali kwa pamoja ili kuinua na kuviendeleza viwanda vyetu hapa nchini, lengo letu lilikuwa kuwawezesha wasindikaji wadogo nchini.
“Si kwamba tumetosheka na mafunzo pekee bali tunaomba na tunazidi kuomba taasisi mbalimbali ili kutuunga mkono kwa suala la viwanda ili kukuza uchumi wan chi.
“Kwa hiyo kwa yeyote atakayeguswa katika hali, basi tunawakaribisha ili kutoa hata mchango wa mawazo kwani kwetu ni faida tosha.
Ingawa wamepata mafunzo ya kutosha ya usindikaji wa vyakula mbalimbali, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya kukosa maeneo maalumu ya kusindika malighafi hizo, ndio maana tuliweza kuwaalika wadau hao ili waweze kutusaidia kwa hali yoyote ile ili tuweze kuondokana na tatizo hili ambalo limekuwa ni kikwazo kwa wasindikaji walio wengi nchini,” anasema Laiza.
Mafunzo na mawazo ya wadau wa taasisi mbalimbali hayatoshi pekee kuwafikisha mahali wanapostahiki kufika, bali kubwa zaidi ni watengewe maeneo maalumu kwa ajili ya viwanda ambayo yatakuwa yamesheheni huduma za kijamii katika kiwanda.
Hamasa iliyotolewa na taasisi hiyo ya kuitaka Serikali na wadau wa taasisi mbalimbali nchini kuweza kutoa mchango wao iweze kuzaa matunda ifikapo mwaka huu ili kuviinua viwanda vyetu na kufikia mahali tunapostahili katika kufanikisha lengo letu, Watanzania kuwa na Tanzania ya viwanda kama kauli na rai ya Rais Dk. Magufuli inavyosema.