25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waislamu watibuka kuzikwa Mahakama ya Kadhi

Waumini wa Kiislamu wakiswali
Waumini wa Kiislamu wakiswali

NA ELIZABETH MJATTA

WAKATI Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, akitarajia kutoa msimamo wake leo kuhusu hatua ya Bunge Maalumu la Katiba kuzika suala la Mahakama ya Kadhi, Waislamu kupitia Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu (Hayat), wameapa kuipigia kura ya hapana Rasimu ya Katiba pindi itakapofika kwa wananchi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Naibu Katibu Mkuu wa Hayat na Mwenyekiti wa Jukwaa la Waislamu la Kuratibu maoni ya Katiba, Sheikh Mohamed Issa, alisema kama Bunge hilo litarudisha Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba kupigiwa kura na wananchi ikiwa haina kipengele cha Mahakama ya Kadhi, wataipigia rasimu hiyo kura ya hapana.

Alisema kitendo cha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walio wengi kutogusia suala la Mahakama ya Kadhi ni mwendelezo wa kuwanyima Waislamu haki yao ya muda mrefu.

“Lakini hili tumeliona toka katika Tume ya Jaji Warioba walipotuambia kwamba suala hili lisiingizwe katika maoni ya Rasimu ya Katiba hadi nchi mbili washirika kwa maana ya Zanzibar na Tanganyika zitakapokuwa na Katiba zao na waliingize suala hili katika katiba hizo,” alisema Sheikh Issa.

Alisema walihoji jambo hilo, lakini majibu yaliyotoka waliona hayakuwa na nia njema katika kuleta Kadhi katika nchi hii.

“Tulipata majibu ambayo yalionyesha kabisa mwelekeo mzima juu ya Kadhi ni ‘negative’, kwahiyo toka ilipoanzia na hapa ilipofikia hatushangai,” alisema Sheikh Issa

Sheikh Issa alisema kwa sasa wataendelea kuhamasishana kwa nia ya kupiga kura ya hapana katika rasimu itakayorudishwa kwa wananchi

“Mimi sielewi kwanini katika nchi hii tunaogopa Kadhi, majirani zetu wa Kenya wameingiza Kadhi kwenye Katiba yao, jambo hili tumeliomba siku nyingi na tuliambiwa tusubiri mchakato wa Katiba, lakini mchakato ndiyo huu na mambo ndiyo hayo yanayotokea,” alisema Sheikh Issa.

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Simba, alipotafutwa na MTANZANIA Jumapili juzi kuhusu suala zima la Mahakama ya Kadhi, alisema angetoa tamko lake jana baada ya kukutana na viongozi wa Baraza la Maimamu (Ulamaa).

“Nimekutana na Ulamaa, katika makubaliano yetu tunasubiri kukutana na wawakilishi wetu wa bungeni watupe taarifa rasmi ili tunapotoa tamko tusije tukapishana wakatulaumu kwamba hatujawashirikisha,” alisema Mufti Simba jana wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusu kikao chake na Ulamaa kilichofanyika juzi.

Wakati Mufti akisema hayo, Msemaji wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania (Forum), Sheikh Rajab Katimba, alisema Waislamu kudai Mahakama ya Kadhi si jambo la huruma bali ni haki yao.

“Mimi nashangaa kwanini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanakataa Kadhi wakati ilikuwa moja ya jambo waliloweka katika Ilani ya chama chao, najiuliza kwanini watu hawa hawa wakati ule waone linafaa na sasa hivi waone halifai, wanataka kutuaminisha kwamba wao ni vinyonga wanabadilika badilika au vipi, lakini wafahamu kabisa kwamba jambo hili ni haki ya Waislamu na wanachofanya ni kuukataa ukweli kwa muda tu,” alisema Sheikh Katimba.

Suala la Mahakama ya Kadhi liliibua mjadala mkali katika vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hadi kuundiwa kamati ndogo iliyokuwa inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu.

Hata hivyo, juzi wakati kamati hiyo ikiwasilisha maoni yake, suala hilo lilionekana kuzimwa kwa sababu ambazo hazikuelezwa bayana.

Ilidaiwa baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo waliweka misimamo ya kutozungumzia suala hilo ingawa baadhi ya wajumbe wachache wa kamati namba nne na tisa waliibua licha ya kutopata mwitikio kama ilivyokuwa katika vikao vya awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles