27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Askari wawili wauawa, SMG 10, risasi na mabomu vyaporwa

IGP Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu

NA PETER MAKUNGA, BUKOMBE

HOFU ya usalama wa raia na mali zao imetanda baada ya askari polisi wawili kuuawa na bunduki 10 aina ya SMG kuporwa katika Kituo Kikuu cha Polisi wilayani hapa.

Uporaji huo umefanywa na watu ambao hawajafahamika baada ya kuvamia kituo hicho saa 9:45 alfajiri na kuwashambulia askari polisi waliokuwa zamu ambapo wawili waliuawa na wengine watatu walijeruhiwa.

Mbali na kupora SMG 10, pia inadaiwa wamefanikiwa kupora risasi ambazo idadi yake haijafahamika, pamoja na mabomu ya kutupa kwa mkono ambayo walitokomea nayo kusikojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uvamizi huo umetokea baada ya askari waliokuwa doria kushambuliwa kwa bomu kupitia dirisha la chumba cha mapokezi (CRO) kituoni hapo na kisha kushambuliwa kwa risasi.

Aliwataja askari waliouawa kuwa ni WP 7106 Uria Mwandiga na G. 2615 PC Dustan Kimati. Waliojeruhiwa ni E.5831 CPL David Ngupama Mwalugelwa aliyejeruhiwa kichwani na usoni huku akiumizwa mdomo na meno mawili kung’oka na Mohamed Hassan Kilomo ambaye amejeruhiwa kifuani na mguu wa kulia.

Mganga Mkuu wa Wilaya

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dk. Honorata Rutatinisibwa, amekiri kupokea maiti za askari wawili na majeruhi wawili.

Alisema hali za majeruhi zilikuwa mbaya, hivyo walihitaji matibabu zaidi na kulazimika kuwahamishia Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.

IGP atua eneo la tukio

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, alilazimika kwenda Bukombe jana akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Geita ikiongozwa na mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa, Saidi Magalula.

IGP Mangu ameagiza askari polisi wa mikoa jirani ya Tabora, Shinyanga,Kagera, Mwanza na Kigoma kushirikiana na askari wa Geita kuwasaka wahusika na kurejesha silaha zote zilizoporwa.

Agizo la IGP kuwataka askari wa mikoa ya jirani kusaidia msako huo, linatokana na asilimia 60 ya eneo la Wilaya ya Bukombe kuwa na misitu mikubwa.

Alisema msako huo utasimamiwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Isaya Mungulu ambaye aliwasili Bukombe kwa helkopta ya polisi saa 11:39 jioni tayari kwa kuanza msako huo.

Pamoja na hayo, IGP Mangu pia alitangaza dau la Sh. milioni 10 kwa mtu atakayesaidia kukamatwa kwa wavamizi hao, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa silaha zilizoibwa.

Katika kile ambacho kilionyesha kwamba viongozi wa juu wa jeshi hilo wamekasirishwa na tukio hilo, jijini Dar es Salaam Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, naye aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea tukio hilo, huku akiwataka wananchi kuwa na utulivu.

Hili ni tukio la pili katika kipindi cha miezi mitatu kwa majambazi kuvamia kituo cha polisi. Juni 11, mwaka huu askari polisi mmoja aliuawa baada ya watu wasiojulikana kuvamia Kituo Kidogo cha Polisi cha Kimanzichana mkoani Pwani kisha kupora bunduki tatu aina ya SMG na risasi zake.

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

  1. Matukio mawili ni zaidi ya shule. tujifunze kwa tukio moja na kuchukua hatua kali zitakazokuwa na jibu la kudumu, matukio yote mawili yamepoteza askali wetu wapendwa.ushauri:tuwache mazoea ya kuingia katika vituo vetu vya polisi venye silaha na risasi kama kwenye duka la bidhaa za kawaida,lazima tukubali dunia ya leo sio ya siku za nyuma,lazima kuwe na cheki point mita kadhaa na askari wa mafichoni wa kujibu mashambulizi.ni ukweli kwa mfano polisi post zilizo nyingi silaha za moto zinaweza kuporwa ata kwa kisu, utawakuta wamekaa katika bench silaha zipo ndani.tuongeze utayari na kuacha mazoea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles