25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wahamiaji haramu sasa watumia treni

Mwandishi Wetu – Tabora

SERIKALI imesema itadhibiti wimbi la wahamiaji haramu wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali nchini kwa treni, huku ikiwataka wananchi kuacha tabia ya kuwahifadhi na kuwasafirisha.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni mkoani Tabora wakati wa kikao na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapo baada ya kuwapo kwa taarifa zinazohusisha baadhi ya wahamiaji haramu kutumia usafiri wa treni kuingia katika mikoa mbalimbali nchini.

“Nchi yetu inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka huu, hivyo ni vyema kudhibiti watu wanaoingia nchini pasi na kufuata utaratibu rasmi, na tuna taarifa juu ya wahamiaji haramu sasa kuanza kutumia njia ya treni kuingia nchini, tena wengine wakisaidiwa na raia. Sasa natoa onyo wenye tabia hiyo kuacha mara moja na vyombo vya ulinzi na usalama viimarishe ulinzi katika maeneo husika,” alisema Masauni.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kaimu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi, Amiru Sadiki aliiomba Serikali kuweka maofisa uhamiaji katika vituo vyote vya reli nchini ili kukagua wasafiri wanaoingia katika mikoa mbalimbali kama ilivyo katika viwanja vya ndege.

Awali akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema hali ni shwari huku kukiripotiwa matukio machache.

“Upungufu wa makosa ya mauaji ambayo hapo awali yalikuwa kero kubwa kwa wananchi, umetokana na juhudi za polisi katika kufanya doria ya kukamata waganga wa kienyeji wanaojihusisha na ramli chonganishi.

“Tayari jeshi tumeanza operesheni maalumu inayoendelea katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Mwanza, Kagera, Simiyu na Tabora huku kukiwa na mafanikio makubwa, na hali sasa inaendelea kutulia,” alisema ACP Mwakalukwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles