25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

WAJUE ‘WANAUME’ SITA WENYE KIU YA KUCHEZA VPL

GLORY MLAY

LIGI Daraja la Kwanza(FDL), imezidi kushika kasi, lakini mvuto zaidi unatokana na timu zinazopambana kwa nguvu kusaka tiketi ya kufuzu Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Tayari timu zimecheza mechi 15, hata hivyo imekuwa ni vigumu kutabiri timu gani itapanda Ligi Kuu, kutokana na matokeo kutotabirika.

Tofauti na msimu uliopita ambapo mapema dalili za timu fulani kufuzu Ligi Kuu kutoka katika kila kundi zilionekana, safari hii unaweza kuamka ukakuta anayepewa nafasi ameteremshwa.

Wakati kila kundi lina timu 12, katika kila kundi kuna timu tatu zaidi ya tatu ambazo zinafanya vizuri.

Mazingira hayo yanafanya kuwepo kwa uwezekano wa timu zitakazopanda Ligi Kuu Bara msimu ujao kufahamika wazi katika raundi ya lala za lala salama.

Ikiwa utaratibu uliotumika msimu uliopita kuamua timu za kupanda Ligi Kuu utatumika msimu huu,  ni wazi ushindani utakuwa mkali zaidi wakati ligi hiyo itakapokuwa inakaribia kutia nanga.

MTANZANIA linakuletea wewe mdau wa soka na msomaji wa gazeti hili, uchambuzi wa timu sita zinazoonekana kuwa ndizo zenye nafasi zaidi ya kufuzu Ligi Kuu msimu ujao kutokana na kasi zilizonayo dimbani.

DODOMA JIJI FC

Ni timu ambayo inaongoza katika msimamo wa Kundi A, ikiwa na pointi 30, baada ya kucheza mechi 15, ikishinda tisa, kutoka sare mbili na kupoteza mechi tatu hivyo kujikusanyia pointi 30.

Timu hiyo ipo chini ya Kocha Mkuu, Mbwana Makatta, ambaye anasema akili na mawazo yake yote awewekeza kwenye michezo ilipo mbele yao kuhakikisha hawashuki walipo kwa sasa.

“Msimu huu ni moto, kila timu inabana matokeo labda mkiwa wajanja kama mmewasoma mapema na kujua mbinu zao hapo mnaweza kupata pointi tatu kwa kutumia makosa yao, bila hivyo hakuna unachopata, ili upate ushindi unatakiwa utumie akili nyingi na sio nguvu,”anasema.

IHEFU FC

Ni timu iliyopanda daraja msimu uliopita, baada ya kufanya maajabu katika mechi zake za Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL).

Timu hiyo imekuwa ikisumbua FDL kutokana na ubora wa wachezaji wake, hivyo timu nyingi zimekuwa zikigonga mwamba na kushindwa kuondoka na pointi tatu muhimu.

Ihefu inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo, baada ya kucheza michezo 15, kushinda tisa, kutoka sare mechi tatu na kupoteza mechi tatu hivyo kujikusanyia pointi 30.

MBEYA KWANZA

Inashika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo ikiwa na pointi 28, baada ya kucheza mechi 15, ikishinda mechi nane, sare mechi nne na kupoteza mechi tatu.

Kocha Mkuu wake, Maka Malwisi, anasema kuwa timu hiyo inapambana kupanda Ligi Kuu na hata ikishindikana ibaki kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

“Hata tukikosa nafasi basi tubakie kwenye nafasi nzuri, ili watu wakiona waseme kwamba kweli walipambana lakini bahati haikuwa yao.

“Tunapambana kuona jinsi gani tutachomoka kwenye hii vita, maana ni kali na kila timu ina silaha za kutosha,” anasema.

GWAMBINA FC

Katika Kundi B, Gwambina inaongoza msimamo, ikiwa imejikusanyia pointi 31, baada ya kucheza mechi 15, ikishinda tisa, ikitoka sare  nne na kupoteza michezo miwili.

Kocha wa timu hiyo, Furgence Novatus, anasema ligi hiyo imekuwa ngumu hivyo lakini watapambana kuhakikisha wanapanda Ligi Kuu msimu ujao.

“Kundi ni gumu, ukifungwa mechi moja aliye nyuma yako anakupita,  anapanda juu wewe unashuka chini, ushindani bado ni mkubwa, ni ngumu kutabiri nani atapanda.

“Lakini tunajiamini tutakuwa miongoni mwa timu zitakazocheza Ligi Kuu msimu ujao,” anasema.

Geita Gold

Inaifukuzia Gwambina, ambapo inashika nafasi ya pili katika msimamo, baada ya kucheza mechi 15, ikishinda mechi saba, sare mechi nne na kupoteza michezo minne hivyo kujikusanyia pointi 25.

Hassan Banyai ndiye kocha Mkuu wa timu hiyo ambaye anasema kila kukicha hali ya hewa inabadilika kutokana na ushindani mkubwa kwenye kundi lao.

Anasema timu inaweza kuongoza siku tatu lakini ikipoteza au kutoka sare nafasi yake inachukuliwa nyingine hivyo zinahitajika juhudi kusalia nafasi za juu.

“Msimu huu ushindani ni mkubwa kwasababu kila timu inataka kupanda.

Tunachotakiwa ni kupambana huku kila siku tukitumia mbinu mpya kuwashinda wapinzani, hakuna timu inayokubali kupoteza mchezo kirahisi, itapambana ihakikishe inaondoka na pointi tatu au moja,” anasema.

Arusha United

Ni timu ya jijini Arusha ambayo imekuwa miongoni mwa timu zinazosaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu.

Ipo nafasi ya tatu kwenye kundi hilo, baada ya kucheza mechi 15, ikishinda sita, sare sita na kupoteza tatu hivyo kujikusanyia pointi 24.

Arusha inanolewa na nyota wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe.

Ulimboka ametamba kuwa atafanya kila njia kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo chanya kwenye michezo yao, ili kukata tiketi ya Ligi Kuu.

“Ligi haitabiriki kila timu inapambana iwezanavyo kuhakikisha inapanda daraja, hata sisi tunapambana tunawapa hamasa wachezaji wasije kukata tama.

Tunatumia kila mbinu kuhakikisha tunapata matoke bora ili kufikia malengo yetu,” anasema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles