HERIETH FAUSTINE NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM
BAADHI ya wafanyabiashara wadogo katika eneo iliyokuwa stendi ya zamani ya Mwenge, wameulalamikia uongozi wao kwa kuwatuhumu kuwatoza ushuru wa Sh1000 kila siku bila kuwapa stakabadhi.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara katika stendi hiyo, walisema wamekuwa wakitozwa ushuru huo bila kujua zinapokwenda.
Mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema wamekuwa wakichangishwa kila siku fedha na viongozi wao.
“Kila siku tumekuwa tukichangishwa ushuru wa shilingi 1000 kwa madai ya kufanya eneo hilo kuwa safi, hatukatai kuchanga hizo fedha lakini tunachojiuliza mbona hatupewi risiti na zinakwenda wapi hizo fedha?” alihoji mfanyabiashara huyo.
Naye mfanyabiashara, Saidi Juma, alisema walikubaliana kutoa Sh1000 kwa ajili ya usafi katika eneo hilo kwa sababu si soko rasmi na halitambuliwi na Manispaa ya Kinondoni.
MTANZANIA liliutafuta uongozi wa soko hilo ili kupata ufafanuzi wa malalamiko hayo ambapo Katibu wa soko hilo, Sharifu Hassan, alisema wameshindwa kutoa risiti hizo za ushuru kutokana na soko hilo kutotambulika na Manispaa ya Kinondoni.
Alisema ni kweli kila siku wafanyabiashara wa soko hilo wamekuwa wakikusanya ushuru wa Sh 1,000 kwa ajili ya usafi.
“Tulikubaliana na wafanyabiahara wa hapa ambao tupo 170, tuwe tunalipa Sh 1000 kwa ajili ya usafi wa eneo hili ambapo shilingi 500 kwa ajili ya ukusanywaji wa taka hizo na Sh 500 nyingine kwa ajili ya uzolewaji taka.
“Na hii hela tulikubaliana wenyewe baada ya uongozi wa Serikali ya mitaa kusema kuwa hawatambui uwepo wetu katika eneo hili,” alisema Hassan.
Alisema kutokana na changamoto zinalolikabili soko hilo, wameiomba Serikali kulirasimisha soko hilo kama masoko mengine ili liweze kuwa chini ya manispaa husika.
“Soko hili limekuwa likiongozwa na sisi wenyewe kwa kila kitu, hivyo tunaiomba Serikali kulifanya liwe rasmi kama lilivyo Soko la Mawasiliano na Makumbusho,” alisema.