Wasomali waandamana kupinga ‘kuporwa’ mpaka na Kenya

0
1026
Yusuf Hussein Jimale
 Yusuf Hussein Jimale
Yusuf Hussein Jimale

MOGADISHU, SOMALIA

MAMIA ya Wasomali walimiminika mitaani mjini hapa juzi kupinga madai ya Kenya kumiliki sehemu ya mpaka wa Bahari ya Hindi, ambao unaaminika kuwa na utajiri mkubwa wa nishati.

Mgogoro huo wa muda mrefu baina ya mataifa hayo jirani ya Pembe ya Afrika, unasikilizwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mjini Hague, Uholanzi wiki hii.

Uamuzi wa ICJ ndio utakaobainisha hatima ya shughuli za utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta katika eneo hilo.

Wakiongozwa na waandamanaji waliojifunga vitambaa vya rangi ya bendera ya Somalia, mamia ya watu walimiminika na kuilaani Kenya kwa hatua yake hiyo.

‘Hakuna mtu anayeweza kununua maji ya eneo la Somalia,” Meya wa Mogadishu, Yusuf Hussein Jimale, alisema wakati akipokea maandamaano hayo katikati ya mji juzi.

“Tuna matumaini makubwa kuwa kesi itatoa uamuzi wa haki utakaokuwa upande wetu,” aliongeza.

Somalia ililifikisha suala hilo ICJ mwaka 2014, ikisema majadiliano ya muda mrefu na Kenya hayakuzaa matunda.

Nchi zote mbili zinadai kwamba eneo la pembe tatu lina ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 100,000, ambalo linaaminika kuwa na utajiri wa gesi na mafuta.

Wakati kesi ikianza kusikilizwa mapema wiki hii, Kenya ilisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwa sababu hiyo, inaitaka itupe ombi la Somalia.

Leo mahakama hiyo itaamua iwapo iitupe au iendelee na kesi hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here