WACHINA wawili na Watanzania wawili, wamekamatwa katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa kosa la kuuza dawa zilizokwisha muda wake.
Watu hao walikamatwa mjini hapa jana wakikwangua karatasi zilizo kwenye chupa za viuatilifu kuonyesha muda wa matumizi ya dawa hizo.
Baada ya kukwangua karatasi hizo, walikuwa wakibandika karatasi mpya kuonyesha dawa hazijaisha muda wake.
Wachina na Watanzania hao walikamatwa na maofisa wa Mkoa wa Mtwara wakiongozwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Khatibu Kazungu.
“Watu hawa wanabandua nembo zilizoisha muda na kuweka nembo mpya kwa ajili ya kuwauzia wakulima.
“Inaonekana huu ni mchezo wao na wanarudisha nyuma wakulima ambao wamekuwa wakitumia pesa nyingi kununua dawa na kupulizia mazao yao wakati zimekwisha muda wake.
“Huu ni ukatili, yaani hivi unawezaje kuwauzia wakulima wa korosho na mazao mengine pembejeo zilizokwisha muda wake?
“Ufike wakati tuwe na huruma kwa wakulima kwa sababu wanahangaika sana kuhudumia mazao yao,” alisema Kazungu.
Naye Ofisa Kilimo wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Steven Macha, alisema tabia hiyo haiwezi kuvumiliwa kwa kuwa inarudisha nyuma maendeleo ya wakulima.
“Tabia hii inasababisha wakulima kutumia gharama kubwa na kupata faida kidogo wakati wa mavuno, hali ambayo imekuwa ikipunguza imani kwa wataalamu wa kilimo.
“Kwa hiyo, nawaomba wakulima na wananchi kwa ujumla, tushirikiane kukomesha tabia hii kwani inaathiri uchumi wa nchi yetu,”alisema Macha.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mtwara, Thobias Sedoyeka, alisema wako makini kukabiliana na mtandao wa wahalifu hao.
“Dawa hizo inaonekana zilitengenezwa mwaka 2013 na zilikwisha muda wake tangu mwaka 2015.
“Dawa hizo hizo zimekutwa katika maboksi zaidi ya 625 yakionyesha dawa zimetengenezwa mwaka huu 2016 na zitakwisha mwaka 2019.
“Hii dawa inaonekana ‘life span’ yake ni miaka mitatu ndio maana wamefanya hivi lakini pia tayari ilikuwa imeshamaliza muda wake wa matumizi hatua ambayo inaweza kuhatarisha mazao mchanganyiko yanayolimwa mkoani hapa….
“Mara kadhaa wakulima wamekuwa wakilalamika kuharibika kwa mazao shambani hii ni hujuma na pia wanatutia umasikini hatuta muacha mtu yeyote aliyehusika katika tukio hili, hawa watu wanamatawi tunafanya utaratibu ili tuweze kuwakamata wote na kukomesha hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa” alisema Sedoyeka.