LONDON, UINGEREZA
SIKU moja tu baada ya kufichuka kuwa bilionea na mmiliki wa Klabu ya Chelsea ya hapa, Roman Abramovich, amekwama Urusi baada ya Uingereza kushindwa kufufua viza yake, wabunge wametaka mabilionea wa nchi hiyo watimuliwe.
Aidha hatua ya Uingereza kushindwa kufufua viza ya kumruhusu Abramovich, imekuja siku chache tu baada ya kuonekana katika orodha ya Rais Donald Trump ya watu wenye shaka, huku uhusiano wa Uingereza na Urusi ukilegalega kufuatia tukio la jasusi wa zamani wa taifa hilo kuwekewa sumu nchini hapa.
Wabunge wamewatuhumu mawaziri kuhatarisha usalama wa taifa wa Uingereza kwa kufumbia macho fedha chafu kutoka Urusi zinazomiminika jijini hapa.
Wabunge hao wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, walisema pamoja na kelele kufuatia shambulio la sumu la Salisbury dhidi ya jasusi Sergei Skripal, Rais Vladimir Putin na washirika wake wanaendelea kutumia jiji hili kufanikisha malengo yao haramu.
Wakihitimisha ripoti yao, wabunge walisema Serikali inahitaji kuonyesha msimamo wa kiuongozi kisiasa kwa kuwawekea vikwazo watu wenye uhusiano na Kremlin na kuziba mianya inayotumiwa kupenyeza fedha chafu.
Kamati hiyo ilisema mali zilizowekezwa na mabilionea hao jijini hapa, zinatumika kusaidia kampeni ya Putin kumjengea taswira kimataifa na kukwaza washirika wa Magharibi.
Walisema kukabiliana na kampeni hii chafu, kunapaswa kuwa sehemu ya sera muhimu ya kigeni ya Uingereza.
Pamoja na jaribio la kutaka kumuua kachero wa zamani wa Urusi, Skripal na binti yake Yulia kutumia sumu aina ya Novichok, ambayo Uingereza inaituhumu Urusi, kamati imesema hali imekuwa ‘biashara kama kawaida’ kwa matajiri wa Urusi walioweka kambi jijini hapa.
Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Chama tawala cha Conservative, Tom Tughendhat, imekuwa ikimbana Waziri wa Mambo ya Nje, Boris Johnson, awakabili mabilionea hao na kuzuia fedha haramu kuingia Uingereza.
Ripoti ya kamati hiyo inakuja huku mmiliki wa Chelsea, Abramovich, visa yake ikiwa haijafufuliwa tangu imalizike mwezi uliopita.
Bilionea huyo hakuhudhuria mechi ya fainali ya Kombe la FA, ambalo timu yake ililitwaa Jumamosi iliyopita.
Vyanzo vya habari karibu na bilionea huyo, vilisema ingawa ombi lake la viza mpya halijakataliwa, mamlaka za Uingereza zinachukua muda mrefu kuliko kawaida kuifufua bila kutoa maelezo yoyote.
Aidha ucheleweshaji huo unakuja wiki kadhaa tu baada ya Serikali kusema inatathmini hadhi za matajiri 700 wa Urusi walioingia kwa viza ya uwekezaji.