RAMADHAN HASSAN– DODOMA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma, imewahoji wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaomaliza muda wao, Livingstone Lusinde (Mtera) na Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini) kwa tuhuma za kuhusika kugawa rushwa kwa wajumbe ili waweze kuungwa mkono kugombea tena ubunge.
Serukamba pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii huku Lusinde akisifika kama mbunge mwenye ushawishi katika kujenga hoja ndani ya Bunge dhidi ya wapinzani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sostenes Kibwengo, alithibitisha kushikiliwa na kuhojiwa wabunge hao wakihusishwa na tuhuma za rushwa kwa kushawishi wajumbe ili waweze kuwania tena ubunge katika majimbo yao.
LUSINDE
Kibwengo alidai kuwa Julai 7, mwaka huu majira ya mchana, waliwakamata watu 20 ambao ni wanachama wa CCM wakiwa nyumbani kwa Lusinde eneo la Mvumi, Wilaya ya Chamwino.
Alidai uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba watu hao na wengine waliofanikiwa kutoroka walifika nyumbani kwa mbunge huyo kupatiwa fedha ili wamsaidie wakati wa vikao vya uchaguzi.
SERUKAMBA
Kibwengo alithibitisha pia kushikiliwa na kuhojiwa kwa Serukamba kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wanachama wa CCM ili kushawishi mambo yanayohusina na uchaguzi.
Alisema Serukamba pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na pia ni mtia nia ya ubunge katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.
MJUMBE WA NEC
Pamoja na matukio hayo, Takukuru Mkoa wa Dodoma pia inamshikilia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Halima Okashi kwa tuhuma za kutoa rushwa ili aweze kupata ubunge wa Viti Maalumu.
Kibwengo alidai kuwa walimkamata mjumbe huyo akitoa rushwa kwa baadhi ya wanachama wa CCM ili wampitishe katika nafasi hiyo.
“Vitendo hivyo vikithibitika ni kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007 na sheria zinazosimamia uchaguzi. Taarifa zaidi zitatolewa pindi uchunguzi ukikamilika.
“Tunawataka wanasiasa na wananchi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa ya uchaguzi kwa kuwa ni kinyume na sheria na vyombo vyote vipo makini kupambana nao,” alisema Kibwengo.