*Sumaye avunja ukimya kwa viongozi
Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
SEKESEKE la orodha ya watumishi walioghushi vyeti limepamba moto huku sekta ya ya afya ikitikiswa zaidi.
Huku hali ikiwa hivyo, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ameweka wazi suala zima wa uhakiki wa vyeti na akitaja sifa ya kiwango cha elimu inayotakiwa kwa wakuu wa mikoa na wilaya.
Sumaye alisema mabadiliko hayo yalifanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu wakati yeye akiwa waziri mkuu na msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali.
Orodha iliyochapishwa kwenye baadhi ya magazeti jana ilionyesha watumishi wa kada mbalimbali ambao wanadaiwa wamekuwa wakitumia vyeti vya kughushi kinyume cha sheria.
Wakati hayo yakiendelea, Zahanati ya Kibada katika Manispaa ya Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam ilitajwa kuwa watumishi wake wamekumbwa na tatizo hilo, hali iliyochangia huduma kuzorota kwa wagonjwa.
MTANZANIA ilifika katika zahanati hiyo jana na kumkuta muuguzi mmoja tu ambaye alisema zahanati hiyo haijafungwa.
Hata hivyo alisema uhakiki huo umewakumba wenzake watatu ingawa idadi kubwa bado walikuwa wakiendelea na kazi kwa mujibu wa utaratibu.
“Si kweli, hatujafunga zahanati, huduma inaendelea kutolewa kama kawaida.
“Kwa kuwa hiki ni kituo kidogo cha afya siku za mwishoni mwa wiki (Jumamosi na Jumapili) baadhi ya idara huwa zinafungwa mapema.
“Pengine wakadhani ni kwa sababu ya vyeti feki, si kweli ni hali ya kawaida, ingawa idara hizo zinawahi kufungwa haimaanishi mgonjwa akija ahudumiwi, anahudumiwa kama kawaida maana kuna huduma za dharura,” alisema.
Alisema katika kituo hicho wapo wataalamu zaidi ya 10 na katika orodha iliyotolewa na serikali ya wenye vyeti vya kughushi, yamo majina matatu ya wenzao.
“Tumeona majina ya wenzetu watatu kwa kweli hata sisi tumeshangaa, bado hatuamini kama ni wao, tunaona pengine kuna ‘typing error’ (makosa ya uchapaji)… huwezi jua naamini serikali ipo makini katika utendaji wake,” alisema muuguzi huyo.
MTANZANIA lilihitaji kuonana na Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo kupata ukweli zaidi lakini hakuwapo ofisini kwa muda huo.
Sumaye
Wakati huohuo, Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, ameweka wazi suala la uhakiki wav yeti feki, alipohojiwa katika kipindi cha Uchumia, Siasa na Utamaduni cha redio moja ya Dar es Salaam.
Alisema akiwa bado Serikalini katika awamu ya tatu yalifanyika mabadiliko kuhusiana na taratibu za utumishi wa umma kwamba kwa wakuu wa mikoa na wa wilaya, lazima viwango vyao vya elimu vianzie Shahada ya Kwanza.
“Nakumbuka katika nafasi ya kuwakilisha watu kama vile wabunge na madiwani ndiyo wanaosema hivyo, kwamba mtu awe anajua kusoma na kuandika, kama wananchi wanawaona wanaweza kutafsiri vizuri na kuwaletea kile walichowatuma kutoka bungeni au kwenye halmashauri.
“Lakini nakumbuka katika taratibu za utumishi siyo hivyo, hayo mabadiliko yalifanyika katika awamu ya tatu…najua katika taratibu za utumishi tulikubaliana kuwa mkuu wa wilaya lazima awe na digrii na ni mahitaji la nafasi hiyo kwa sababu pamoja na kuwa ni shughuli za siasa pia anasimamia shughuli za utendeji ambazo nyingi ni shughuli utaalamu za Serikali.
“Hivyo hauwezi kusema DC na RC awe anajua kusoma na kuandika…kusema awe anajua kusoma na kuandika tu,” alisema
Alisema pengine walifanya hivyo wakati wa uhuru, lakini anachojua walifanya mabadiliko.
Sumaye alisema kwenye nafasi za utendaji kama mkuu wa wilaya na RC hauwezi kubadilisha, hivi sasa hata makatibu tarafa wengi ni wale waliomaliza chuo kikuu.
Alisema akiwa serikalini kama Waziri Mkuu ulipitishwa utaratibu ambao mkuu wa wilaya lazima awe na shahada ya kwanza.
“Haiwezekani leo katika umri huu tuseme mkuu wa mkoa awe anajua kusoma na kuandika. Hivi kweli inaingia hata akilini?
“Hapa ni kwamba kilichofanywa ni kumlinda mtu fulani.
“Hatuwezi kuwa na utaratibu kwamba mradi mtu akiwa anajua kusoma na kuandika anaweza kuwa mkuu wilaya na mkoa… hata kuwa katibu tarafa hatufai,” alisisitiza Sumaye.