Asha Bani –Dar es salaam
WAZIRI wa Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amesema Serikali imesitisha safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwenda Afrika Kusini kuhofia usalama wa abiria na ndege zenyewe kwa sababu ya vurugu zinazoendelea nchini humo.
ATCL iliyoanza safari zake kwenda Afrika Kusini hivi karibuni, ilizisitisha Agosti 21, mwaka huu baada ya ndege ya Serikali aina ya Airbus A220-300 inayotumiwa na shirika hilo, kushikiliwa nchini humo kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng kutokana na kesi ya fidia iliyofunguliwa na mkulima Hermanus Steyn dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Ndege hiyo ilirejea nchini juzi usiku baada ya kesi ya mkulima huyo kutupwa na Mahakama Kuu ya Gauteng.
Jana akizungumza Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Kamwelwe alisema licha ya ndege hiyo kuachiwa, wanasheria wa Serikali wamebakia nchini humo kukazia hukumu ili mshtaki aweze kulipa gharama za kesi kama alivyoelezwa na mahakama.
Alisema wameamua kusitisha safari za kwenda nchini humo kutokana na usalama wa ndege wakihofia vurugu zinazoendelea nchini humo kwa wazawa kupiga wageni kutoka nchi nyingine za Afrika pamoja na kuharibu mali zao.
“Kwa sasa hatuwezi kupeleka ndege huko mpaka pale taifa hilo litakaposema hali imetulia na ituhakikishie usalama wa ndege yetu na usalama wa abiria watakaotumia chombo hicho pia.
“Ila mashirika mengine hayazuiwi kupeleka abiria nchini humo, ni ATCL tu, na taarifa hizi kwa undani tayari mwakilishi wangu, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Elias Kandikwa nimemtuma kuwaeleza wabunge kuhusu suala hilo.
“Naamini pia wananchi watapata taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu yanayoendelea na hatua mbalimbali zilizofikiwa,” alisema Kamwelwe.
Alisema jana asubuhi wataalamu walikagua ndege iliyokuwa imeshikiliwa Afrika Kusini na kuona iko salama, hivyo iko tayari kwa safari nyingine ambazo ilitarajiwa kuzianza jana mchana.
“Tanzania imefanikiwa katika usafiri wa anga na itasonga mbele, wenye maneno maneno watashindwa.
“Rais (John) Magufuli anatuagiza, sisi tunatekeleza, na tutafanya kazi. Ndege nyingine zinaingia Novemba, Watanzania wasiwe na hofu, tupo imara zaidi na tumeyashtua mataifa mengi kwa mafanikio,” alisema Kamwelwe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe, alisema waliposikia kuhusu suala la kuzuiwa kwa ndege ya ATCL Afrika Kusini waliumia.
“Jambo hili hata sisi lilitushughulisha na kutuuma kutokana na kuona kwamba Serikali imeleta ndege na wenzetu wamefanya yao huko Afrika Kusini, lakini tunashukuru Mungu imeachiwa kwa sasa tusonge.
Mara baada ya kushikiliwa kwa ndege hiyo nchini Afrika Kusini, Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi alisema; “kesi hii ni madai ya muda mrefu ya fidia ya ardhi iliyotwaliwa tangu miaka ya 1980 huko, hivyo si kesi kwamba ni ATCL ndiyo inadaiwa, Hapana. Tunaipambania ndege hii kwa masilahi ya taifa letu na tunaamini siku moja itarudi kuendelea na shughuli zake za kawaida.”
Maombi ya kupinga kushikiliwa kwa ndege hiyo nchini Afrika ya Kusini yalisikilizwa Ijumaa iliyopita.
Katika kesi hiyo, mawakili kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, walishirikiana na mawakili wa Afrika Kusini katika maombi ya kupinga kushikiliwa ndege hiyo.
Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa juzi na mahakama hiyo ambayo gazeti hili imeiona, Agosti 30, Serikali iliwasilisha sababu tatu za kupinga kushikiliwa ndege hiyo ikidai kwamba tozo ya kulipa dola za Marekani milioni 36 ilikufa baada ya kufikia makubaliano ya kulipa dola za Marekani milioni 30.
Ilidai katika hoja zao, Steyn hawezi kutumia tuzo ya kwanza ya kumlipa dola za Marekani milioni 36 kufungua kesi ya kushikilia mali nchi ya kigeni.
Pia Steyn hawezi kulazimisha kusaini makubaliano nchini Afrika Kusini.
Hoja ya pili ni kwamba kinga ya dola inazuia ukamataji wa mali za dola hata kama unaidai, ikiwa suala lililowaleta mahakamani si la kibiashara.
Inadaiwa makubaliano kati ya Serikali na Steyn si zao la biashara kama wakili wake alivyodai mahakamani.
Katika hoja ya tatu ni uraia wa wahusika wa kesi hiyo kwamba, Tanzania na Steyn hawana uwezo kisheria kuzitumia mahakama za Afrika Kusini kwa kuwa wote sio raia wa nchi hiyo.
Mahakama ilikubali hoja moja ambayo ni ya kwanza kati ya hoja tatu zilizowasilishwa na kuona kwamba haina mamlaka ya kushikilia mali hiyo, hivyo kuamuru iachiwe na Steyn alipe gharama za kesi pamoja na za mawakili wawili wa upande wa Serikali.
Hoja nyingine mbili mahakama haikuzijadili katika kutoa uamuzi wake.