23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mahakama yatoa neno kesi masheikh wa Uamsho

Kulwa Mzee -Dar es salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imempa njia mbili Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ikimshauri kukamilisha haraka upelelezi ama kuiondoa kesi ya ugaidi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed na wenzake 21.

Pia imeondoa zuio kwa waandishi wa habari kuandika mwenendo wa kesi hiyo kwa sababu haijafikia hatua ya usikilizwaji, hivyo wanaruhusiwa kuiripoti.

Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde, ilitoa uamuzi huo jana baada ya kukubaliana na maombi ya washtakiwa katika kesi hiyo.

Washtakiwa kupitia mawakili wao, Abubakar Salim, Juma Nassoro na wengine, waliwasilisha maombi mawili mahakamani.

Ombi la kwanza waliomba mahakama imshauri DPP kukamilisha upelelezi ndani ya mwezi mmoja na la pili iondoe amri ya kuwazuia waandishi wa habari kuripoti kesi hiyo.

Akitoa uamuzi, Hakimu Maira alisema mahakama inampa njia mbili DPP, moja kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ndani ya muda mfupi na ya pili kama anaona kuna sababu za upelelezi kuchelewa kukamilika, aliondoe shauri hilo mahakamani, atakapokuwa tayari atawashtaki tena.

“Katika maombi ya kuondoa amri ya kuripoti  kesi hiyo, mahakama inaondoa amri hiyo, hiyo amri ilitolewa bila kudhamiria kwa sababu kifungu namba 34 cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi kinahusu mamlaka ya Mahakama Kuu.

“Mahakama Kuu ndiyo inaweza kutoa amri hiyo kwa sababu sheria inazuia kuandika jina na kutoa picha ya shahidi wakati wa usikilizaji wa kesi.

“Kwa hatua iliyofikia kesi hii, usikilizwaji bado, hivyo waandishi wanaruhusiwa kuingia na kuandika kwa lengo la kutenda haki,” alisema.

Kesi hiyo namba 29 ya mwaka 2014 ilifunguliwa mahakamani hapo Agosti mwaka 2014.

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Faraja Ngoka.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya  kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.

Mbali na Sheikh Farid, Washatakiwa wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassani, Hussein Ally, Juma Juma.

Wengine ni Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro, Said Sharifu, Sheikh Mselem Ali Mselem na Abdallah Said Ali.

Wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni mwaka 2014, washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.

Inadaiwa katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, Sheikh Farid aliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.

Pia Sheikh Farid anadaiwa kuwa kwa makusudi na akijua, alitoa msaada kwa watu hao wa kutenda vitendo vya kigaidi kinyume na sheria. Pia anadaiwa kuwa katika kipindi hicho akiwa anajua kuwa Sadick na Farah wametenda makosa ya kigaidi, aliwahifadhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles