JUZI ilikuwa kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Kumbukumbu hiyo ilifanyika nchi nzima kwa njia na matukio tofauti yaliyohudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali.
Sisi wa MTANZANIA Jumapili tunaamini kuwa Watanzania wengi bado wanampenda na kumkumbuka Mwalimu Nyerere si kwa sababu alikuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika. La hasha! Kwa sababu nchi nyingi duniani zilipata kuwa na marais wao wa kwanza lakini haziwaenzi kama tunavyofanya sisi.
Tunaamini Watanzania wataendelea kumkumbuka Mwalimu Nyerere kwa sababu alijali utu wa watu wote na katu hakutumia madaraka yake kujinufaisha kama walivyofanya marais wengine wa Afrika na hata Amerika ya Kusini.
Pia tunafahamu kuwa baada tu ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mwalimu Nyerere aliweka wazi kwamba alikata kutengeneza nchi isiyojali dini, rangi, ukanda ama ukabila. Baada ya Uhuru wapo baadhi ya Waafrika wakati ule waliotaka nafasi zote za uongozi wapewe watu ‘weusi’. Wako pia waliowaona watu ‘weupe’ kama ni maadui zao kwa kuwa walishabihiana na wakoloni wa Uingereza ambao chama cha TANU wakati ule ndio walikuwa wamewashinda katika sakata la kudai uhuru.
Baadhi ya Waafrika wenzetu wakati ule walitaka Nyerere atengeneze sheria za kuwapendelea zaidi wazawa Waafrika na kuwakandamiza wengine. Lakini akiwa rais wa kwanza Nyerere alikataa katakata jambo hilo na ndiyo maana kwa miaka yote aliendelea kupendwa na watu wote.
Ndio maana wakati mwili wake ulipowasili Dar es Salaam ukitokea London, Uingereza alipofariki dunia Oktoba 14, 1999, watu wa jamii zote wakiwamo watu wa jamii zote walifurika Uwanja wa Ndege kumpokea huku wakibubujikwa na machozi. Mwalimu Nyerere hakuipata heshima ya Watanzania kwa bahati mbaya. Matendo yake, kujishusha kwake, upendo wake na msimamo wake katika mambo ya msingi kama umoja, amani, ulinzi, kilimo vilimpa heshima.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amewahi akinukuliwa akisema kuwa Mwalimu Nyerere aliongoza kwa mfano.
Alishirikina na wananchi kwa kushika jembe na kulima, kufyatua matofali na kufyeka maeneo ya pori.
Hata wakati wa ujenzi wa Ikulu Ndogo ya Chamwino mjini Dodoma, Mwalimu Nyerere alishiriki kikamilifu katika ujenzi wake. Kiongozi huyo mzoefu, anawashangaa viongozi wa sasa kwa kutembelea mashamba huku wamevaa suti!
Kimsingi, tunafahamu kuwa mengi yamesemwa juu kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha Mwalimu Nyerere lakini kubwa ni wito kwa viongozi wa sasa wamuenzi kwa vitendo. Wanasiasa wengi wanadai kumuenzi Mwalimu Nyerere lakini hiyo haitakuwa na maana kama viongozi haohao kwa matendo yao wanahatarisha uhai wa Muungano.
Tunafamu katika moja ya mambo makuu ambayo Mwalimu Nyerere aliyatetea kwa nguvu zake ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania mwaka 1964.
Kitendo chochote cha kuuchokonoa Muungano ni kujitenganisha na Mwalimu Nyerere bila kujali wewe ni kada wa CCM au vyama vya upinzani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amewaita wanafiki wale wanaosema wanamuezi Mwalimu Nyerere huku matendo yao ni ya kuvunja Muungano.