Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam |
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wa chama hicho watano wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka manane yakiwamo kushawishi watu kuandamana na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Aquillina Akwilini.
Katika mashtaka hayo, Mbowe pekee amesomewa mashitaka matano yakiwamo mawili ya uchochezi na kusababisha uasi.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi amesema washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa kufanya mkusanyiko isivyo halali wenye kuchochea vurugu hata baada ya kutolewa tamko la kusambaratika waliendelea.
Amedai washtakiwa hao walishawishi watu kuandamana na kusababisha uvunjifu wa amani na watu kuichukia nchi.
Amedai maandamano hayo yalisababisha kifo cha mwanafunzi huyo na watu kujeruhiwa wakiwamo askari sita.
Hata hivyo, Wakili Nchimbi aliiomba Mahakama isitoe dhamana kwa washtakiwa hao kwa usalama wa umma wa Watanzania.