BANGUI, AFRIKA YA KATI
JESHI la Umoja wa Mataifa (UN) la kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, limesema moja ya vituo vyake vilishambuliwa kwa risasi wakati yalipozuka mapambano kati ya makundi mawili yanayohasimiana.
Mapigano yaliibuka juzi Jumatatu baina ya makundi hasimu yaliyomeguka kutoka lililokuwa kundi la waasi wa Seleka, katika mji wa Bria, kilometa 400 kaskazini mashariki mwa Bangui.
Vituo vya jeshi hilo vilishambuliwa na Chama cha Wananchi kwa Mwamko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (FPRC) kabla ya kuondolewa kutoka eneo hilo baada ya mapambano ya risasi.
FPRC ni kundi lililojitenga kutoka Seleka likiongozwa na Noureddine Adam ambaye anakabiliwa na vikwazo kutokana na madai ya kushiriki mauaji ya mwaka 2013 na 2014.
Kundi jingine lililotokana na waasi hao na lililohusika na mapigano hayo ni Muungano kwa ajili ya Amani ya Afrika ya Kati (UPC) linaloongozwa na Ali Ndarass.
Jamhuri ya Afrika ya Kati, moja kati ya nchi masikini zaidi duniani, imekuwa ikihangaika kurejea katika hali ya kawaida tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipoibuka mwaka 2013 baada ya kundi la Seleka kumpindua Rais Francois Bozize.