NA PENDO FUNDISHA
-MBEYA
Vigogo wawili waliowahi kuwa wakurugenzi wa Jiji la Mbeya, Jumanne Rashid na Mussa Zungiza wamefikishwa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, na kusomewa mashitaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara.
Washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo Agosti 17, kuunganishwa na wenzao sita waliofikishwa mahakamani hapo jana kwa makosa kama hayo.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite, mwendesha mashitaka wa serikali Shadrack Martin aliwasomea mashtaka hayo ambapo hawakutakiwa kujibu kitu na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 29, mwaka huu huku dhamana yao ikifungwa.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Elizabeth Munuo, Meya wa Jiji, Athanas Kapunga, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Samweli Lazaro, Mhasibu Mkuu wa Jiji, James Joligiki, Mhasibu Msaidizi, Tumaini Msigwa, na Msimamizi wa Idara ya Ujenzi, Henry Mganga.