23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

SIKU 60 ZA VIGOGO IPTL SEGEREA

NA KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

UPELELEZI wa kesi ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani milioni 22 na Sh bilioni 309, inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engeneering & Marketing, James Rugemalira na mwenzake haujakamilika.

Hadi sasa ni siku 60 tangu vigogo hao wafikishwe mahakamani kwa mara ya kwanza na kupelekwa Gereza la Segerea, Dar es Salaam baada ya kukosa dhamana.

Rugemalira ambaye ni mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL),  na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Ltd (PAP), Harbinder Singh Sethi, walipanda kizimbani jana kwa mara nyingine kwa kesi yao kutajwa.

Akiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi kuwa kesi ilikuwa inatajwa na upelelezi haujakamilika.

Washtakiwa waliwakilishwa na mawakili wanane, huku sita kati yao wakimwakilisha Sethi akiwamo Joseph Mwakandege na Rugemalira akiwakilishwa na wawili; Didas Respicius na Chuma John.

Wakili Swai, aliomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine na kupendekeza iwe Agosti 31 kwa sababu Magereza waliomba iwe hivyo kutokana na utaratibu waliopanga kuleta watuhumiwa.

Mahakama ilikubaliana na maombi hayo na kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe hiyo kwa kutajwa.

Katika kesi hiyo, Sethi na Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi; yakiwamo kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa Rugemalira na Sethi kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 Dar es Salaam, walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka la pili, wanadaiwa kujihusisha na mtandao. Kwamba, kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014, Dar es Salaam wakiwa si watumishi wa umma walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Shtaka la tatu, Sethi anadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio, Ilala, Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.

Seth katika shtaka la nne anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera kwa nia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka la tano, washtakiwa wote, wanadaiwa kati ya Novemba 28/29, 2011 na Januari 23, 2014 Makao Makuu ya Benki ya Stanbic, Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la St. Joseph, kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Katika shtaka la sita la kusababisha hasara, washtakiwa wanadaiwa kuwa Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati, Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Katika la saba, kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja wanadaiwa kuwa walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300.27 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Shtaka la nane, wanadaiwa Novemba 29, 2013 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Tanzania, Wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola 22,198,544.60 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Shtaka la tisa, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14, 2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic, Kinondoni, Dar es Salaam, alitakatisha fedha, Sh 309,461,300,158.27 kutoka BoT wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Shtaka la kumi, inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemalira alitakatisha fedha, Sh 73,573,500,000 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la 11, inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemalira alitakatisha fedha Dola za Marekani 22,000,000 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.

Shtaka la 12, Sethi anadaiwa Januari 28, 2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic, Wilaya ya Kinondoni, alihamisha Rand za Afrika Kusini 1,305,800 kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika Standard Bank Land Rover Sandton Johannesburg, wakati akijua katika kipindi anahamisha fedha hizo, zimetokana na zao la kujihusha na genge la uhalifu.

Hata hivyo, Sethi aliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, lakini juzi aliamua kuyaondoa kupitia kwa mmoja wa mawakili wake, Melkzedeck Lutema kwa sababu aliwahusisha mawakili wa nje ya nchi katika kumtetea kwenye maombi yake hayo.

Mawakili hao kutoka Afrika Kusini hawana cheti kinachowaruhusu kufanya kazi katika mahakama za hapa nchini, kutoka kwa Jaji Mkuu, jambo ambalo linawafanya wakose sifa ya kumwakilisha mshtakiwa huyo.

Ingawa mawakili hao hawakuwa wametambulishwa mahakamani hapo, majina yao yametajwa kwenye hati za maombi ya dhamana ya mshtakiwa huyo.

Juzi Wakili Lutema aliomba kuyaondoa maombi hayo kwa lengo la kuyafungua upya.

 

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Hao mjadala uxiwepo kinachotakiwa waende ndan,wafilisiwe na not ze2 zirud haiwezekan wa2 waish kama wapo pepon na familia zao halafu weng wa watanzania wanaish maisha ya hovyo kabsa hawaijui kesho yao itakuwaje,wachache kama hao wala peke yao wakat wanyonge mitaan na vjjn wanakimbizwa na polx migambo ili walpixhwe kod wakat wanamaisha magumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles