26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI LUCKY VINCENT KUTUA LEO KIA

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

WANAFUNZI watatu wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya jijini hapa ambao walinusurika kwenye ajali ya basi wilayani Karatu Mei 6, mwaka huu, wanatarajiwa kuwasili leo nchini.

Mapokezi ya wanafunzi hao, yanatarajiwa kuongozwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye hata hivyo kwa sasa yupo nchini Afrika Kusini kwenye mkutano wa dharura wa SADC, akimwakilisha Rais Dk. John Magufuli.

Watoto hao, Sadia Ismail, Doreen Mshana na Wilson Elipokea, wanatarajiwa kurudi nchini wakitokea Marekani, walipokuwa wakitibiwa baada ya kupata ajali hiyo iliyosababisha vifo vya wanafunzi 31 wakiwamo walimu wawili na dereva.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), alisema watoto hao watapokewa leo asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Makamu wa Rais ndiyo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi ila taarifa nilizopata leo (jana), huenda akawakilishwa na Mkuu wa Mkoa ila sijajua wa Arusha au Kilimanjaro,” alisema Nyalandu.

Alisema kuwa watoto hao wanatarajiwa kutua katika uwanja huo na ndege aina ya Samaritan Purse DC 8, saa 3 asubuhi ambayo imeondoka jana mchana katika mji wa Charlotte, Jimbo la North Carolina ambapo itakuwa angani kwa saa 18 hadi kufika Kilimanjaro.

Kiongozi huyo aliwaomba wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kujitokeza kupokea watoto hao waliopo na wazazi wao, na kuwa ndege hiyo ikishatua watoto hao watakabidhiwa mashada ya maua na wanafunzi wenzao wa Lucky Vincent.

“Akina mama watakabidhiwa mashada ya maua na waume zao ambao walibaki nchini, waliotoa ndege wametuma ujumbe wa watu 16, mwakilishi wao mmoja atapewa taji pamoja na Jeniffer na Calvin ambao walihusika na kuokoa watoto siku ya ajali, watapewa mashada pia,” alisema.

Aliwataja wengine watakaokuwapo ni mjumbe wa Baraza la Congress, Steve King, mke wake na baadhi ya wajumbe na  daktari bingwa wa mifupa, Dk. Steve Meyer, aliyeongoza jopo la wataalamu kuwahudumia watoto hao.

Nyalandu alisema katika mapokezi hayo, nyimbo za taifa za Tanzania na Marekani zitaimbwa na waimbaji wa injili; Angel Benard wa Tanzania, huku wimbo wa Marekani ukiimbwa na Mercy Masika kutoka Kenya.

“Baada ya kuwapokea kutakuwa na salamu mbalimbali ikiwemo kutoka kwa watoto hao, viongozi wa dini, Serikali na wazazi,” alisema.

Kwa mujibu wa Nyalandu, watoto hao pamoja na familia zao, baada ya kupokewa wataelekea katika Kijiji cha Stemm kilichopo eneo la Mbuguni, nje kidogo ya Jiji la Arusha ambako watalala huko kwa uangalizi wa madaktari hadi kesho watakapopelekwa kuungana na familia zao.

“Kabla ya kueleka majumbani mwao, wataenda kutembelea shule yao na mchana watarudi Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mt. Meru watakapokutana na madaktari waliokuwa wanawahudumia ambako pia watakabidhi  vifaa vya matibabu hospitalini hapo, vilivyopatikanaa nchini Marekani,” aliongeza.

Akizungumzia gharama za matibabu zilizotumika kuwatibu watoto hao, alisema kwa sasa hawezi kujua ila ni kubwa akitolea mfano gharama ya ndege hiyo.

“Ndege kama hii wanasema inagharimu Dola za Marekani 300,000 kwa gharama ya kwenda na kurudi, kulikuwa na ndege nyingine ndogo ambazo zilikuwa zikiwachukua pale Marekani, gharama ni kubwa, lakini zimetolewa na watu tofauti  na kwingine watu wamejitolea.

“Serikali ilituma daktari na muuguzi mmoja wakaenda na wale watoto ambapo pia ilibeba jukumu la kuwahudumia pamoja na gharama za kuwatunza wakiwa kule,” alisema Nyalandu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles