WATAFITI kutoka nchini Uswizi wamethibitisha kwamba glasi moja ya bia huwafanya watu kujuana zaidi na kufunguka roho.
Kundi la watafiti kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Basel, wamefanya utafiti kwa watu 60, nusu wakapewa bia na wengine wakapewa kinywaji kingine, ambacho si bia. Kisha watu hao wakashiriki katika matukio tofauti tofauti.
Mtafiti Mkuu, Profesa Matthias Liechti, anasema kuwa watu wanaokunywa bia kwa wastani ni wachangamfu, hushirikiana na kujuana na wenzao vema kuliko wale ambao hawanywi bia.
Pia imethibitishwa kuwa wanaokunywa bia hushirikiana kwa pamoja masuala mengi na kwamba kinywaji hicho husaidia kutuliza mawazo, lakini lazima utumiaji wa mvinyo usiwe wa kupindukia.
Mapema mwaka huu, Serikali ya Uingereza ilitoa masharti mapya ya utumiaji wa mvinyo. Ushauri wa serikali ulipendekeza raia wasinywe zaidi ya glasi saba za mvinyo au bia.
Masharti haya yalitolewa baada ya ushahidi kuonyesha kwamba unywaji pombe kupindukia unahatarisha mtu kupata saratani ya matiti.
Lakini utafiti huo unasisitiza kuwa kunywa pombe kunamfanya mtu kuwa na furaha, pia kujizuia na kufanya ngono kiholela.
Chanzo: BBC