23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 10, 2022

Je, unajua kwamba asilimia 100 ya warembo Venezuela ni feki?

warembo-venezuelaJOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM

UNAPOLITAJA taifa linalotawala kwa fani ya urembo au kwa maneno mengine malkia wa urembo duniani bila shaka fikra zako hazitakupeleka kwingine zaidi ya Venezuela, wengine wataelekeza fikra hizo India.

Ndiyo, yote hayo ni mataifa yanayofanya vyema katika tasnia hiyo lakini Venezuela ikiwa kinara.

Taifa hilo la Amerika ya Kusini lenye utajiri wa mafuta limetoa warembo sita wa dunia (Miss World), saba wa Miss Universes, sita wa Miss Internationals na wawili wa Miss Earths.

Lakini pia kama utadhani kuwa mafanikio hayo yametokana na kujaliwa na Mwenyezi Mungu wingi wa mabinti warembo kuliko mataifa yote duniani utakuwa umekosea.

Naam, mafanikio yake hayo yamekuja kwa gharama kubwa mno kifedha na kimwili au kimateso-lazima kisu au sindano ipite katika miili ya mabinti hawa ili kupata urembo ule utakiwao.

Wadau wa tasnia hii huwaambia wasichana wenye umri wa miaka hadi 12 kurekebisha makalio yao, kuchongwa pua zao na wale wenye umri wa miaka 16 kupandikizwa matiti.

Wasichana wengine hupitia visu kuondoa mafuta, pia utumbo wao mdogo ili kuwezesha kuchakacha chakula kwa kasi.

Na Wi May Nava, aliyeshiriki Miss Venezuela mwaka 2013, alikiri kuwa alilazimika kupachikwa kwa kushona kipande cha plastiki(mesh sewn) katika ulimi wake ili kumzuia kula vyakula vigumu. Hilo lilienda sambamba na upandikizaji wa matiti, kurekebisha meno na pua.

Inaaminika njia ya mesh sewn katika ulimi husaidia kudhibiti ulaji holela na hivyo mhusika kutonenepeana, ikitumika zaidi Amerika ya Kusini kama muafaka kwa upunguzaji uzito.

Wazazi pia huwachoma sindano watoto wao wenye umri wa miaka minane au tisa kwa homoni zinazochelewesha kuvunja ungo na hivyo kuwafanya wakue warefu.

“Ndoto ya kila msichana wa Venezuela ni kuwa Miss Venezuela,” mwanaharakati Taylee Castellanos anasema.

“Hawahimizi tena uasili wa mwanamke. Wanahimiza wanawake ambao kwa asilimia 100 ni feki, yaani waliotengenezwa upya miili kinyume na ile waliyobarikiwa.

Castellanos (32) mkazi wa Maracay, ni msemaji wa kundi linalopinga vitendo hivyo NO to Biopolymers, YES to Life, ambalo huonya wasichana kuhusu hatari ya sindano ya kemikali ya silicone ili kuongeza ukubwa wa makalio.

Wanaharakati wanapinga vyuo vyenye nguvu vya urembo ambamo wasichana hutiwa moyo kukubali upasuaji na kuwafundisha wasichana wadogo kutembea mwendo wa kipaka (catwalk).

Chuo cha Belankazar, kinachojulikana kama ‘Kiwanda cha Warembo’ kikongwe zaidi katika mji mkuu wa taifa hilo Caracas, kimezingirwa na ofisi wa upasuaji wa plastiki. Wasichana 600 wanaonekana wakiwa katika hatua ya mwisho ya kumaliza shule.

Castellanos kamwe hakuwahi kuwania taji lolote la urembo lakini alifanyiwa upasuaji mwaka 2010, ambao ulimzuia kutembea.

Kundi lake la kiharakati linapingana na mawakala wa urembo, shule za urembo ambazo mara nyingi hulaghai familia kutafuta njia ya kuondokana na umasikini.

“Miss Venezuela si mfano mwema kwa wanawake,” Castellanos alisema. “Hufanya kila kitu halali kwa haramu ili kupata mwonekano ule wautakao.”

Lakini Mkurugenzi wa Belankazar, Alexander Velasquez, anasema shule za aina hiyo ni nzuri kwa Venezuela na zinahimiza taswira nzuri ya mwanadamu.”

Alikiri kwamba sehemu kubwa ya wanafunzi wake, wazazi wao ni wale wa kipato cha chini — mara nyingi wa kipato cha dola 50 sawa na Sh 110,000 kwa mwezi. Nusu ya kipato hicho huishia katika gharama za ada, nguo na vipodozi.

“Siamini kuwa Venezuela ina wanawake wazuri kuliko wote duniani, lakini tuna utaalamu wa utengeneza wanawake wazuri zaidi, warembo na kamilifu,” Velasquez aliliambia gazeti la Daily Mail.

“Na ndio maana tunatamba sana kwenye mashindano yote makubwa ya urembo duniani.”

Mdau mwingine wa fani ya urembo, Bruno Caldieron, ambaye anamiliki vibali saba vya mashindano ya urembo Venezuela, alishuhudiwa akimruhusu mmoja wa wanamitindo wake kuwekwa mkanda wa plastiki kuzunguka kiuno chake ili kukipunguza kutengeneza umbo la namba nane.

Mkanda huo kwa mujibu wa waliowahi kuwekewa ni mchungu mno.

“Iwapo tumbo la msichana haliko kamili, anapaswa kulirekebisha,” Caldieron alisema. “Iwapo pua yake haivutii, anapaswa kuirekebisha.”

Yorgelys Mero, mwanafunzi katika Chuo Cha Belankazar mwenye umri wa miaka 15 anasema walimu wake walimtaka atengeneze pua yake.

Msichana huyo anayeishi katika nyumba duni inayoelekea kuanguka anaishi na bibi yake ambaye hulipa vifaa vya kurekebisha meno na ambaye amejiandaa kutafuta mkopo kwa ajili ya upasuaji.

“Watu wengi wameniambia kuwa nahitaji kurekebisha pua,” Mero alisema. “Ila nadhani mimi ni mzuri kwa jinsi nilivyo. Lakini iwapo hicho ni kitu cha lazima ili nifike juu, nitakuwa tayari kukifanya,” alisema.

Lakini harakati hizo za kujitengeneza mdoli ili kufanana na washindi wa mataji ya dunia ya urembo – mara nyingi huishia pabaya.

Makumi ya wasichana hufa kila mwaka wakati wa upasuaji katika taifa hilo.

Hivi karibuni kuna kampeni ya kuwaelimisha wasichana wa Venezuela kuhusu hatari ya kemikali ya majimaji ya kupandikiza makalioni (silicone) kabla ya kufikisha umri wa miaka 12, ambapo wazazi mara nyingi huenda mbali kuwatunuku binti zao zawadi ya kufikisha umri wa miaka kwa sindano za kurekebisha maumbile.

Mwasisi wa taasisi ya NO to Biopolymers, YES to Life, Mary Perdomo alifariki dunia miaka sita iliyopita ikiwa ni matokeo ya sindano hizo makalioni.

Ndoto za kila msichana kuwa ‘Miss’ kwa imani kwamba ndio uanamke kamili na njia ya kuelekea mafanikio makubwa kitaifa na kimataifa katika tasnia ya urembo na mitindo zimejikita nyoyoni mwa wasichana wengi.

Unapoishi katika taifa ambalo mwanamke mrembo hupata mafanikio kikazi kutokana na mikataba minono kuliko yule mwenye utaalamu wa kazi au msomi, unajikuta ukizama katika fikra kuwa hakuna kilicho muhimu kuliko urembo.

Kwamba Venezuela imezalisha washindi wengi zaidi katika mashindano makubwa ya dunia kuliko taifa lolote lile duniani na hivyo kuifanya tasnia hiyo kuwa kitambulisho na fahari ya taifa.

Kwa sababu ya mitazamo na imani hizo, wanaharakatui wanapingao urembo wa kutengeneza wana kazi kubwa ya kupiga vita mwenendo huo wenye madhara ya kiafya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles