MOSCOW, URUSI
SERIKALI ya Urusi imelaani vikali shambulizi la Ijumaa iliyopita katika msikiti uliopo eneo la Sinai mjini hapa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 235, na kwamba iko tayari kushirikiana na Misri kuwasaka magaidi waliofanya unyama huo.
“Tunalaani kwa nguvu zote shambulizi hilo la kigaidi lililotokea katika eneo la Sinai, Misri. Urusi mara zote imekuwa ikipinga vikali mashambulizi yoyote ya kigaidi bila kujali nia na uwezo wa wataalamu au itikadi zao za uhalifu,” ilieleza taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje.
“Wakati tukisikitika kwa unyama huu na kutoa pole kwa serikali ya Misri na watu wake, tuko tayari kujitolea kushirikiana nanyi kuwasaka wahalifu hawa,” taarifa hiyo iliendelea kueleza.
Katika mshambulizi hilo ambalo lilitokea mwishoni mwa wiki watu wapatao 235 walipoteza maisha na wengine 130 kujeruhiwa wakati walipokuwa wanatoka msikitini.
Eneo la Sinai hukumbwa na mashambulio ya mara kwa mara yanayofanywa na wanamgambo wanaoipinga Serikali ya Misri, na msikiti uliolengwa ni maarufu kwa waumini wa madhehebu ya Sufi na watu wa kabila la -Sawarka wanaosemekana kuunga mkono kikamilifu Serikali ya Rais rais Abdel-Fattah al-Sisi .