PORTO, URENO
TIMU ya taifa ya Ureno, imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mataifa ya UEFA baada ya kuwachapa wapinzani wao Uholanzi bao 1-0, huku Ureno ikiongozwa na nahodha wao Cristiano Ronaldo.
Bao la pekee la Goncalo Guedes lililofungwa katika dakika ya 60, liliweza kuzima ndoto za Uholanzi kutwaa ubingwa huo.
Safu ya ulinzi ya Uholanzi ilionekana kuwa bora hasa kwa kumzuia mshambuliaji hatari duniani Ronaldo na waliweza kufanikiwa kumzuia kucheka na nyavu, lakini walishindwa kumzuia Guedes.
Hata hivyo, kocha wa Uholanzi, Ronald Koeman, amewamwagia sifa Ureno huku akidai walistahili kuwa mabingwa kutokana na kile walichokifanya.
“Mchezo ulikuwa mgumu kila upande, timu zote zilikuwa zinahitaji ubingwa, lakini Ureno wamefanikiwa kutokana na ubora wao pamoja na mbinu, uzoefu wao umewasaidia kwa kiasi kikubwa.
“Mwaka 2016 walikuwa mabingwa wa michuano ya Euro, hivyo wamekuwa na uzoefu mkubwa wa michuano kama hii, lakini wachezaji wangu walipambana kwa kiasi kikubwa ila walikosa bahati,” alisema kocha huyo.
Mara ya mwisho kwa Brazil kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ilikuwa 2007, hivyo mwaka huu wameonekana kuwa na lengo kubwa la kutwaa ubingwa huku mchezo wao wa ufunguzi ukitarajiwa kupigwa Jumamosi wiki hii dhidi ya Bolivia.