NAIROBI, KENYA
MUUNGANO wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), umesema utaandaa mkutano sambamba kesho wakati Rais Uhuru Kenyatta akiapishwa.
Mkutano huo utafanyika kwenye Uwanja wa Jacaranda, Embakasi mjini hapa.
Mkutano huo, ambao maafisa wa polisi wanasema si halali huenda ukasababisha makabiliano makali kati ya wafuasi wa upinzani na polisi
Tayari viongozi wa upinzani wamesema hawatambui ushindi wa Kenyatta kwa madai kuwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Novemba 26 ulikuwa haramu.
Aidha kiongozi mwenza wa NASA, Musalia Mudavadi amesema kuwa watatumia njia halali zilizopo kupinga ushindi wa Kenyatta licha ya kuidhinishwa na Mahakama ya Juu.
Mudavadi pia amewataka Wakenya kutohudhuri sherehe ya kesho ya kuapishwa kwa Kenyatta itakayofanyika kwenye Uwanja wa Michezo Kasarani, badala yake kuhudhuria mkutano wa upinzani ili kuomboleza mauaji ya watu waliouawa na polisi.
Lakini katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi mjini Nairobi, Japhet Koome alisema muungano huo haujaiarifu polisi kuhusu mkutano huo.
“Hatujui lolote uwapo wa mkutano huo. Kwa hiyo iwapo kuna mtu anayedhani anaweza kufanya mkutano bila kuiarifu polisi, mwambieni kuwa sheria itakabiliana naye vikali,” alisema Koome.