23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘MUGABE ALILIA ALIPOCHUKUA UAMUZI WA KUJIUZULU’

HARARE, ZIMBABWE


ALIYEKUWA Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe alilia na kuomboleza kusalitiwa na watu wake wa karibu wakati akikubali kujiuzulu, gazeti la The Standard la hapa limeandika jana.

Mugabe (93) alijiuzulu wakati wa wiki ya mwisho aliyokabiliwa na shinikizo kubwa zaidi kutoka jeshi na chama tawala cha ZANU-PF baada ya miaka 37 madarakani.

Gazeti hilo lilikariri chanzo cha habari kilicho karibu na Mugabe kikisema kiongozi huyo mkongwe alishikilia rozari, huku akifuta machozi wakati akiwaeleza wasaidizi wake wa karibu na timu ya wasuluhishi katika kasri lake la ‘Blue House’ mjini Harare kuwa hatimaye anajiuzulu.

Mugabe alitangaza uamuzi huo wakati bunge likisikiliza hoja iliyowasilishwa na chama chake ya kumng’oa madarakani baada ya awali kugoma kufanya hivyo.

 

“Alitazama chini na kulalamika kuwa watu wake walikuwa vinyonga,’ moja ya vyanzo vivyo vya habari kilikaririwa kikisema.

Lakini pia gazeti linalomilikiwa na Serikali la Sunday Mail lilisema Padri Fidelis Mukonori, aliye karibu na Mugabe ambaye alikuwa mtu wa kati wakati wa majadiliano ya kumshinikiza  ajiuzulu, alisema uso wa kiongozi huyo mkongwe ‘uling’aa’ baada ya kusaini barua ya kujiuzulu.

‘Hivyo hatuzungumzii kuhusu mtu mchungu. Nilimwambia ilikuwa vyema kwake sasa kushuhudia mtu mwingine akiongoza nchi,” Mukonori aliliambia Sunday Mail.

Si Mukonori wala wasaidizi wa karibu wa Mugabe waliopatikana kufafanua suala hilo.

Kwa sasa Rais Emmerson Mnangagwa, mfuasi mtiifu wa zamani wa Mugabe, ambaye aliapishwa Ijumaa iliyopita, anasubiriwa kuona iwapo serikali yake itahusisha mawaziri wa enzi za Mugabe au watu wapya  ikiwamo wapinzani.

Anguko la Mugabe lilitokana na hatua yake ya kumtimua Mnangagwa, umakamu wa rais wakati akiongoza mbio za kumrithi ili kumsafishia njia mkewe Grace (52), kitendo ambacho kilifanya jeshi liingilie kati.

The Standard, gazeti binafsi ambalo limekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Mugabe na serikali yake kwa miaka mingi limemtaka Mnangagwa kutovumilia ufisadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles