25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Upinzani, chama tawala wadai kushinda DRC

KINSHASA, DRC

USHIRIKA wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) umesema mmoja wa wagombea wake atashinda uchaguzi wa rais kwa kuzingatia matokeo ya awali, lakini ule wa chama tawala nao umedai kushinda.

Madai hayo kinzani yanafuatia uchaguzi wenye vurugu uliofanyika juzi, ambao Wacongo milioni 1.2 walishindwa kupiga kura kutokana na mlipuko wa Ebola, migogoro na matatizo ya usafirishaji katika majimbo matatu.

Uchaguzi huo unalenga kumpata mrithi wa Rais Joseph Kabila anayeondoka baada ya miaka 18 madarakani na huenda ukaipatia nchi hiyo ya Afrika ya Kati mabadiliko ya kwanza ya kisiasa kwa njia ya kidemokrasia.

Lakini pia matokeo yoyote yatakayobishaniwa yanaweza kusababisha marudio ya vurugu zilizoshuhudiwa katika uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011.

Vurugu hizo zilidhoofisha hali ya usalama, hasa maeneo ya mpakani mwa DRC na Rwanda, Uganda na Burundi, ambako makundi kadhaa ya wapiganaji yanaendelea na shughuli zao za uasi.

Vital Kamerhe, meneja kampeni wa mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi, alisema hesabu za mwanzo zinamuonesha mgombea wao na mwingine mkuu wa upinzani, Martin Fayulu wakikabana koo kwa kuongoza kwa asilimia 40 ya kura kila mmoja.

Alisema mgombea wa muungano unaotawala, Emmanuel Ramazani Shadary, anayeungwa mkono na Rais Kabila, alikuwa na asilimia 13 tu, ingawa sehemu kubwa ya kura bado haijahesabiwa.

Hata hivyo, Nehemia Mwilanya, mkuu wa shughuli za Ikulu wa Rais Kabila, ambaye pia ni mmoja wa wajumbe wa timu ya kampeni ya Shadary, aliuambia mkutano wa habari jana asubuhi kwamba wana uhakika mgombea wao ameshinda, ingawa hakutoa takwimu.

Kambi ya Fayulu bado haijatoa takwimu mahsusi, lakini mwenyewe alisema juzi jioni kuwa kambi ya Shadary ilikuwa ‘inaota’ iwapo inadhani itashinda uchaguzi huo.

Kura ya maoni ya hivi karibuni iliyochapishwa na taasisi ya utafiti wa DRC ya Chuo Kikuu cha New York Ijumaa iliyopita, ilionesha Fayulu, meneja wa zamani wa kampuni ya mafuta ya Exxon Mobil, alikuwa akiongoza kwa asilimia 47. Tshisekedi alikuwa na asilimia 24 na Shadary asilimia 19.

Matokeo ya kwanza ya awali yanatarajiwa kutolewa na Tume ya Uchaguzi (CENI) leo.

Siku ya uchaguzi ilikuwa tulivu kwa sehemu kubwa licha ya matukio kadhaa ya vurugu, ikiwemo ugomvi katika kituo cha kupigia kura mashariki mwa DRC ambako watu wasiopungua watatu waliuawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles