30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

UPEPO WABADILIKA

Na MWANDISHI WETU

MWELEKEO wa vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya aliyoianzisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, sasa unaweza ukabadilika baada ya Rais Dk. John Magufuli kumteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Kuteuliwa kwa kiongozi huyo, Rogers Sianga ambaye atakuwa na wasaidizi wawili ambao ni Kamishna wa Operesheni, Mihayo Msikela pamoja na Kamishna wa Intelijensia, Fredrick Kibuta, kunatarajiwa si tu kupanua wigo wa vita hiyo bali jambo hilo sasa kuratibiwa kwa taratibu zote za kisheria na mamlaka hiyo.

Uteuzi wao huo umekuja ikiwa ni takribani wiki moja sasa baada ya Makonda kuendesha operesheni hiyo kwa mtindo wa kutaja hadharani majina ya watuhumiwa na kuwataka kufika Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi.

Mtindo huo anaoutumia Makonda katika operesheni hiyo, umeibua maneno mengi huku watu wa kada mbalimbali wakiwamo wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakimpinga vikali.

Wakosoaji dhidi ya mtindo huo wa Makonda, wamekuwa wakisema kinachotakiwa ni Rais kuteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya ili abebe msingi wa kisheria ili kuendesha vyema vita hiyo kama sheria mpya ya kupambana na dawa za kulevya inavyotaka.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema kuwa wateule wataanza kazi mara moja baada ya kuapishwa kesho.

Mapema wiki hii baada ya kuibuka hoja ya dawa za kulevya na jinsi Makonda anavyolishughulikia jambo hilo, Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, alikumbusha umuhimu wa kuunda mamlaka hiyo kama sheria mpya ya kupambana na dawa za kulevya inavyoagiza.

Bulaya ni sehemu ya chimbuko la kuundwa kwa Mamlaka ya kupambana na biashara ya dawa hizo kutokana na hoja binafsi aliyoiwasilisha bungeni mwaka 2013.

Katika hoja yake aliyoitoa mapema wiki hii, alisema kimsingi hapingani na vita dhidi ya dawa za kulevya lakini akashauri wale wote wanaotaka kupambana wasimwogope Rais bali ashauriwe amteue kamishna wa chombo hicho kama sheria inavyoagiza.

Bulaya ambaye pia ni Waziri Kivuli katika Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia dawa za kulevya, alisema yeye, Mbunge wa Kigamboni Dk. Faustine Ndungulile na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Muhagama, ndio waliokuwa mstari wa mbele kushinikiza kutungwa kwa sheria hiyo.

 “Sisi ndio tulianza huu mchezo, tutakapohakikisha hiki chombo kinapata kamishna wa kumsaidia Rais tutakamata wale wanaoingiza dawa za kulevya wale mapapa, hawa wanaokamatwa sasa hivi ni waathirika wanatakiwa kupelekwa Muhimbili, Mwananyamala wakapate tiba.”

Kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo, mapambano hayo yalikuwa yakiongozwa na chombo maalumu kilichokuwa chini ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamishna Godfrey Nzowa, ambaye kwa sasa amestaafu.

Juni 2015, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya na Usafirishaji Haramu, alisema ametia saini sheria mpya ya dawa za kulevya ya mwaka 2015, ambayo ilitarajiwa kwenda sambamba na kuundwa kwa Mamlaka itakayoongoza vita hiyo.

“Sheria hii mpya nina hakika kabisa itasaidia kutokomeza mianya ya uingizwaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya nchini,” alisema Kikwete.

Alisema sheria hiyo itazaa taasisi hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuwakamata na kuwashtaki wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo, huku ikishirikiana na DPP na mhusika akikamatwa atafungwa kifungo cha maisha jela.

Alisema anaondoka madarakani huku sheria hiyo ikiwa tayari imeanza kufanya kazi na atahakikisha inapitishwa mapema ili Rais ajaye akute taasisi hiyo imeanza kazi.

“Sheria hii ambayo tayari nimeshaweka saini ina majibu yote ya Watanzania waliokuwa wakijiuliza kwa miaka yote kuhusu mianya inayotumika kuingiza dawa hizi haramu nchini. Pia, ni sheria itakayotupatia ufumbuzi wa matatizo ya sasa na miaka ijayo itazaa taasisi itakayoratibu, kupambana, kukamata, kupeleleza na hata kupekua ikibidi ili kutokomoza janga hili,” alisema Kikwete.

Alisema ili kupambana na hali hiyo, Serikali imeimarisha vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya sambamba na tume ya kudhibiti na kupambana na dawa hizo, polisi ambao wamepewa mamlaka ya kukamata wafanyabiashara na watumiaji wa dawa hizo.

Hata hivyo, azma yake hiyo haikuzaa matunda kwani sheria hiyo sasa ndiyo itaanza kufanya kazi baada ya kuteuliwa kwa viongozi wa Mamlaka ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.

Mbali na Rais Magufuli jana kuteua viongozi wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, pia alimteua Dk. Anna Makakala, kuwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji. Kabla ya uteuzi huo, Dk. Makakala alikuwa Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji Moshi, mkoani Kilimanjaro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles