Katika siku tatu zilizopita watu 47 wameuawa na wengine 181 kujeruhiwa katika machafuko yanayoendelea mjini Tripoli Libya na viunga vyake huku ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikitoa onyo kuwa mashambulizi hayo dhidi ya raia na miundombinu yao yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) miongoni mwa waliouawa tisa ni raia wakiwemo madaktari wawili ambao wamekuwa wakitoa huduma muhimu kwa raia wanayoihitaji mjini Tripoli, huku mmoja wa madaktari ameripotiwa kuuawa wakati akiwa katika huduma za dharura kwenye gari la kubebea wagonjwa.
WHO inasema imeorodhesha zaidi ya mashambulizi 46 ambayo yameathiri wahudumu wa afya na vituo vya afya kote nchini Libya kwa mwaka 2018-2019 mashambulizi ambayo yamekatili maisha ya wahudumu wa afya na wagonjwa wanane na kujeruhi wengine 24.
WHO imeongeza kuwa, “hali tete inayoendelea, makombora yanayovurumishwa kila uchao na mapigano vinatishia maisha ya raia na kuwa kikwazo kikubwa kwa wahudumu wa masuala ya kibinadamu. Na kuendelea kwa mashafuko hayo Libya mamia ya vituo vya afya vimefungwa na zaidi ya hospital 20 zimeharibiwa au kufungwa.”