26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

UMUHIMU WA KUZINGATIA MUDA UNAPOFANYA MAZOEZI

Dk. Fredirick L Mashili, MD,PhD.


SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) linashauri kufanya mazoezi kwa angalau nusu saa kwa siku. Unaweza kufanya mazoezi kwa muda wa nusu saa kwa wakati mmoja au unaweza kuugawa muda huo katika vipindi vifupi vifupi visivyopungua dakika 10 kila wakati. Hadi hapa unaweza ukawa unajiuliza ni kwanini nusu saa  na endapo nitaugawanya muda huu kwanini dakika 10 na si tano?

Tunapofanya mazoezi kunakuwapo mabadiliko ya kifiziolojia (ufanyaji kazi wa mwili) katika miili yetu. Mabadiliko haya ni pamoja na mapigo ya moyo kuongezeka, kasi ya kupumua kuongezeka na hata mzunguko wa damu kuongezeka. Haya ni mabadiliko muhimu ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo husababisha faida za kiafya zitokanazo na mazoezi. Lakini ndani kabisa yako mambo mengine yanayotokea katika mwili pale tunapofanya mazoezi. Mambo haya yanahusisha kutumika kwa virutubisho mbalimbali kama vile sukari, mafuta na protini.

Wengi wetu tunafanya mazoezi ili kuifanya miili yetu itumie na kuchoma chakula cha ziada tunachokuwa tumekula. Chakula hiki hutumika mwilini kama sukari, mafuta na protini. Mara nyingi pia tunafanya mazoezi ili tutumie chakula kilichotumiwa mwilini kama mafuta. Hii hutusaidia kupunguza mafuta mwilini na kuondokana na madhara yanayoweza kusababishwa na uzito uliokithiri. Lakini kabla ya yote ni muhimu tufahamu kwanza mwili huanza kutumia virutubisho hivi mwilini katika nyakati tofauti. Tutumie mfano wa kukimbia kwa mwendo mdogo (jogging), zoezi ambalo hutumiwa na watu wengi kuelezea kile kinachotokea mwilini.

Unapoanza kukimbia kwa mwendo mdogo (jogging) mwili wako huanza kutumia sukari iliyo katika damu. Sukari hii hutokana na vyakula vilivyoliwa ndani ya saa takribani mbili kabla ya kuanza mazoezi. Kama utaendelea kukimbia ndani ya dakika tatu hadi tano, mwili wako utaacha kutumia sukari iliyo katika damu na kuanza kutumia ile iliyotunzwa katika misuli na ini, ambayo kitaalamu huitwa glycogen. Hii hutumiwa kwa takribani dakika nane hadi 10. Baada ya dakika kumi kama utaendelea kufanya mazoezi mwili wako huanza kutumia mafuta yaliyotunzwa mwilini mwako.

Hii inamaanisha kwamba endapo utafanya mazoezi kwa dakika tano na kupumzika, utakuwa hujafanya mazoezi kufikia muda wa kutumia mafuta. Kwa maana hiyo, mwili wako utakuwa bado haujachoma na kupunguza mafuta mwilini. Hii ndiyo sababu unashauriwa kufanya mazoezi kwa muda usiopungua dakika kumi, zaidi unapaswa ufikishe angalau dakika 12 hadi 15 kama kiwango cha chini. Hii itakupa fursa ya kuchoma mafuta angalau kidogo. Kwa kutumia ufahamu huu, tunatakiwa pia tusibadilishe aina ya zoezi kabla ya kufikisha kati ya dakika 10 hadi 15.

Kumbuka hapa tunazungumzia mazoezi ya aerobics yanayolenga zaidi kupunguza mwili. Wengi wetu hukosea na kufanya mazoezi mengi ndani ya muda wa dakika 10. Mfano mtu anaweza kuanza na baiskeli kwa dakika nane, kasha akapumzika. Baadaye akaanza kukimbia kwa dakika tano na kubadilisha tena zoezi. Mtu huyu hatapata matokeo ya haraka endapo nia yake ni kupunguza uzito.

Lakini pia ili kuufanyisha moyo na mapafu mazoezi ya kutosha, inakupasa kufanya mazoezi mfululizo kwa angalau dakika kumi. Tofauti ni kama unafanya mazoezi ya nguvu kama vile kunyanyua vyuma au kukimbia mbio kwa mwendo kasi. Hapo unaweza kufanya kwa muda mfupi zaidi. Ni muhimu kutimiza muda kamili kila unapofanya mazoezi. Hii itakusaidia kupata matokeo chanya uliyojipangia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles