WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema lazima mashirika ya umma kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF).
Waziri Ummy, alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ulanga, Gudluck Mlinga (CCM) ambaye alihoji ni kitu gani kinashindikana kwa mashirika hayo kujiunga na NHIF.
“Ninawathibitishia mashirika ya umma kujiunga na NHIF si hiari,nimetoka kufanya mazungumzo na na Waziri wa Fedha. Lazima tutumie bidhaa na huduma zinazozalishwa na Serikali,”alisema Ummy.
Awali akiuliza swali lake la msingi, Mlinga alihoji hadi sasa ni taasisi na mashirika ya umma mangapi yamejiunga na mfuko huo na mashirika mangapi hayajajiunga na mfuko huo.
Akijibu swali hilo, Dk. Kigwangalla alisema ni kweli mfuko huo NHIF ulianzishwa kwa ajili ya kuratibu na kusimamia matibabu kwa watumishi wa serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini.
“Hadi kufikia Machi,mwaka huu, idadi ya wanachama katika mfuko ni 792,987 kutoka wanachama 474,760 mwaka 2012. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010, mfuko umefanya maboresho mbalimbali ya vitita vya mafao na namna ya kuchangia kwa makundi mbalimbali ya jamii.
“Maboresho haya yamewezesha kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wanachama walio katika mfumo huu wa bima ya afya nchini na kufanya manufaika kufikia asilimia nane,”alisema.
Alisema hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu, idara za serikali, taasisi na mashirika ya umma zinazotumia huduma za bima ya afya za NHIF zimefikia 307.
Alisema idadi hiyo imetokana na jitihada za makusudi za kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwa watumishi wa umma.
Aliyataja mashirika, taasisi na idara za serikali ambayo hayajajiunga na mfuko huo yapo 23 yakiwemo TRA, BoT, Tanesco, NHC, TPA, PSPF, LAPF,PPF, EWURA, NCA na GEPF.
Kutokana na hilo, alisema mfuko huo unaendelea na jitihada za kukutana na uongozi wa mashirika hayo ya umma kwa lengo la kutoa elimu na kuwahimiza juu ya umuhimu wa kujiunga kama ilivyoainishwa katika sheria ya mfuko.