AVELINE KITOMARY
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inamwewatoa hofu wananchi kutokana na taarifa zilizoenea ya kupatikana kwa wagonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi hatari vya Corona Mkoani Kilimanjaro.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu zilisema kuwa mnamo Machi 13 mwaka huu katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) wasafiri sita walipokelewa wakitokea nchini Kenya.
“Ninapenda kutumia fursa hii kuwatoa hofu wananchi hadi sasa nchi yetu hakuna mgonjwa wa maambukizi ya virusi vya Corona (COVID 19), Wasafiri hao Walikuja kwa ndege ya Precious Airv PW722, wageni hao wanne walikuwa raia wa Denmark na wawili ni raia wa Norway wanawake walikuwa watano na wanaume mmoja.
“Hata hivyo baada ya ukaguzi wa joto la mwili (screening) uliofanywa na maofisa wetu wa afya katika kiwanja hicho waligundua mmoja wao kuwa na homa ya nyuzi joto 38 pamoja na kikohozi na kuchoka,” ilisema Taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia ilisema kuwa wasafiri hao walitengwa na kupelekwa kwenye eneo maalum la kuwatenga washukiwa wa magonjwa ya mlipuko katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro(Mawenzi).
“katika kuwahoji zaidi wasafiri hawa , maafisa wetu walibaini kuwa msafiri mmoja alikuwa na historia ya kukohoa lakini hakuwa na homa hata hivyo wasafiri wote sita walichukuliwa sampuli kwa kuwa walikuwa wakisafiri wote pamoja ambapo sampuli hizo zilipelekwa kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyopo Dar es Salaam kwaajili ya uchunguzi .
“Uchunguzi wa maabara ulibaini kuwa wasafiri wote hawakuwa na maabukizi ya virusi vya corona aidha msafiri aliyekutwa na joto kali alibainika kuwa na mafua ya kawaida hadi sasa hali za wasafiri wote wako salama na wameruhusiwa kufanya shughuli zao.
Hata hivyo taarifa hiyo ilitoa rai kwa wananchi kutokusambaza taarifa ambazo hazijathibitiswa na serikali .