Mwandishi wetu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu leo amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa sekta ya afya kwa lengo la kujadili kwa pamoja tishio la mlipuko wa ugonjwa wa corona.
Waziri Ummy amesema kikao hicho waliwaeleza wadau kama taarifa ya shirika la afya duniani(WHO) ilivyotangaza hali ya maambukizi ya ugonjwa huo duniani hivyo kama serikali ni vyema kuwapatia taarifa wadau hao
“Tumewapa taarifa wadau wetu na kuwahakikishia kwamba Tanzania hakuna mtu mwenye maambukizi mwenye maambukizi ya virusi wa corona na tumewaeleza hatua gani kama serikali tumezichukua katika kujiandaa kukabiliana na tishio hili”.
Katika kikao hicho waziri ameeleza kwamba wizara yake imeweza kuchukua hatua ya kukabiliana na tishio hilo kwa kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye viwanja vya ndege na viingilio vingine ikiwemo bandarini.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kwamba wameweza kutoa mafunzo kwa baadhi ya wataalamu wa afya waliopo mikoani pamoja na kuandaa dawa, vifaa na vifaa tiba endapo nchi itapata mshukiwa wa virusi vya corana.
“Tumewaomba washirikiane nasi katika kuhakikisha kwamba sasa tunakuwa tayari kukabiliana na tishio hilo hata kama hatuna mgonjwa hii tulikuabaliana kwenye mkutano wa nchi wanachama wa SADC kwamba nchi zote tunaingia kwenye hatua ya kukabiliana,”. amesema Waziri Ummy.