23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Nguvu za kiume; tatizo la wazee lililohamia kwa vijana

Aveline Kitomary -Dar Es Salaam 

TAFITI za kisayansi zinaonesha kuwa tatizo la nguvu za kiume hapo mwanzo lilikuwa likiwakumba watu wenye umri mkubwa kwa maana ya wazee, yaani kupungua kwa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa lilikuwa ni jambo la kawaida kwao. 

Lakini, kwenye Dunia ya sasa mambo yamebadilika, tatizo hili halipo kwa wazee peke yao bali hata kwa vijana wenye umri mdogo. 

Ukosefu wa nguvu za kiume limekuwa ni tatizo linalowachanganya vijana kila siku hivyo, muda wote wamekuwa wakihaha kutafuta na kupata suluhisho. 

Ingawa inaweza kuwa tatizo kama matatizo mengine, lakini asilimia kubwa ya wanaume huchukulia upungufu wa nguvu za kiume kama ni suala linalofedhehesha na hata kuona aibu kujieleza hadharani. 

Tafsiri hizo zimefanya baadhi yao kutafuta matibabu ya tatizo hilo kwa njia yoyote ile bila kujali madhara yanayoweza kutokea kiafya baada ya matumizi ya dawa wanazopewa. 

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa matangazo kuhusu uuzaji wa dawa za kuongeza nguvu za kiume yanazidi kukithiri kila kukicha. 

Wengi wa watu wanaoweka mabango hayo ni wale wanaojiita wataalamu wa dawa za asili, ambapo wengine hawajathibitishwa na Mamlaka ya dawa na Vifaa Tiba (TMDA). 

Wakati dawa zinazotambuliwa na mamlaka hiyo ni Viagra, Ericto, Cialis na Suagra ambazo hupatikana katika maduka ya dawa na mgonjwa anatakiwa kuzitumia baada ya kushauriwa na daktari. 

UKUBWA WA TATIZO 

Utafiti uliofanywa mwaka 2016 na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, unaonesha asilimia 24 ya wanaume wana tatizo la nguvu za kiume. 

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti Dk. Pedro Pallangyo, anasema utafiti huo ulifanyika kwa wanaume 18,441 huku umri wa waliochunguzwa ni miaka 47. 

“Tulibaini kuwa asilimia 60 ya wanaume wote walikuwa na uzito kupindukia huku wanane kati ya 100 walikuwa na kisukari na asilimia 61.5 walikuwa na shikizo la juu la damu,” anasema Dk. Pallangyo. 

Utafiti huo ulikuwa mdogo hivyo, ndani ya mwezi huu Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR), inatarajia kuanza kufanya utafiti mwingine ukijumuisha maeneo mbalimbali nchini. 

Mkurugenzi wa Kuratibu na kukuza utafiti, Dk. Paul Kazyoba, anasema utafiti huo utaanzia jijini Dar es Salaam. 

“Tunachotaka kufanya ni kuangalia ukubwa wa tatizo ukoje hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam, watu wanalalamika wakisema jiji hili ndio limekithiri, lakini inawezekana kabisa sio hapa tu, bali hata maeneo mengine tatizo ni kubwa. Tutazunguka maeneo mengi ili kujiridhisha na kutoa takwimu sahihi,” anasema daktari huyo. 

Dk. Kazyoba anaeleza kuwa katika utafiti huo wataangalia zaidi chanzo cha ukosefu wa nguvu za kume, muda wa tatizo kuanza na tiba ambayo zinaweza kumsaidia mhusika. 

“Tukizungumzia nguvu za kiume kuna mambo mengi lazima tuulize, limeanza lini au kama alizaliwa akiwa na shida hiyo tutaangalia vitu vyote ambavyo viliweza kuanzisha tatizo, yapo mambo yanayosababisha yote hayo mfano, kupanda kwa sukari, msongo wa mawazo, kuzaliwa na tatizo, aina ya chakula na masuala ya kisaikolojia,” anabainisha. 

Hata hivyo, anaishauri jamii kuepuka matumizi ya dawa hasa za kuongeza nguvu za kiume ambazo hazijapimwa na kusajiliwa kisheria. 

“Madhara ya matumizi ya dawa zisizopimwa au kuangaliwa usalama wake ni makubwa zaidi ya ukosefu wa nguvu za kiume. Unapotumia dawa ambazo hazijapimwa maana yake unajitoa mhanga kupata tatizo lingine kubwa kuliko kutibu lile ulilonalo. 

“Dawa nyingine zina sumu nyingi hivyo zinaweza kuharibu figo, huwezi kuchukua tu dawa ukanywa kiholela, hata zinazotolewa hospitalini ukitumia bila utaratibu ni lazima zitakuletea madhara ndio maana watu wanaelekezwa namna ya kutumia ili iwasaidie badala ya kumuangamiza. 

“Wito wangu ni kwamba watu wajali afya zao, wafanye mazoezi, waondoe msongo wa mawazo, kupata mlo kamili, wasitumie dawa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika na hata kupimwa na ubora wake. 

“Mamlaka za udhibiti ziangalie jambo hili kwa ukaribu zaidi, ni vizuri watusaidie kudhibiti dawa za nguvu za kiume ambazo hazijafanyiwa utafiti,” anafafanua. 

SONONA YAONGOZA 

Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo na Uzazi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Deogratius Mahenda, anasema asilimia 90 ya wanaume wenye tatizo la sonona ndio wanaokabiliwa na upungufu wa nguvu za kiume. 

Anaeleza kuwa asilimia zingine zilizobaki ni wale wanaokabiliwa na magonjwa ya presha, kisukari na mgongo ambayo yanaathiri mfumo wa damu. 

“Ili nguvu za kiume zitokee mwanamume anatakiwa kuwa na hisia na msichana au maumbile yake kukamilika kama mishipa ya damu kuwa sawa kwenye uume. 

“Inapotokea mtu anapata matatizo ya akili, sonona, huwa anakosa furaha, hisia wala matamanio hivyo kusababisha uume kushindwa kusimama. 

“Inawezekana hata mtu akiwa na mpenzi, mwanzoni walikuwa vizuri lakini baadae ikatokea kutokuelewajna, kisaikolojia anakuwa hata akimwona hapati matamanio naye hata kama ni mke wake analala naye kitanda kimoja hawezi kupata hisia zitazosababisha uume wake kusimama,” anaeleza Dk. Mahenda. 

Anataja kundi jingine la wanaume waliopo hatarini kukosa nguvu za kiume kuwa ni wale wanaofanya kazi sehemu zenye joto kali kutokana na joto hilo kuathiri korodani na hivyo kusababisha uzalishaji wa mbegu hafifu. 

Kwa mujibu wa daktari huyo, kundi la wanaume hao ni wanaofanya kazi za udereva hasa wale ambao magari yao injini zake zina joto kali, wanaofanya kazi viwanda vya kuyeyusha vyuma, matanuru ya kuyeyusha vioo na plastiki. 

“Kwa kawaida, mtu anatakiwa awe na maumbile yaliyosawasawa yenye uwezo wa kupitisha mbegu na korodani zinazozalisha mbegu bora, mifumo hii ikitokea hitilafu inaweza kusababisha mwamume kushindwa kutungisha ujauzito. 

“Mazingira yanaweza kuleta athari kwenye mfumo wa uzazi, kwa kawaida korodani ziko nje kutokana na kuhitaji joto kidogo kwahiyo, kitu chochote kitakachosababisha joto kali kwenye korodani huwa kinahatarisha afya ya mhusika,” anaeleza Dk. Mahenda. 

Anataja sababu zingine za ukosefu wa nguvu za kiume ni magonjwa ya mishipa ya damu (Varicas vain) ambayo husababisha damu kukaa kwa wingi kwenye korodani na kupata joto kali. 

“Pia kuna virus vinavyoitwa mamus, hivi huanza kwa kuvimba mashavu, ikitokea kabla ya mvulana kubalehe au msichana kuvunja ungo hufanya kiwanda cha uzalishaji mbegu kukwama kabisa hivyo watu kama hawa wanatakiwa kutibiwa. 

“Kingine ni korodani kujinyonga na ikatokea isitibiwe haraka kabla ya saa sita, huathirika na kusababisha kutoweza kutengeneza mbegu. 

“Kuna magonjwa yanayoambukizwa kwa kujamiiana kama kisonono ambao husababisha maumivu makali, usaha kutoka kwenye njia ya mkojo na kuacha makovu yanayoweza kuzuia mbegu zisipite,” anabainisha. 

Anaeleza kuwa unywaji wa pombe na ulevi kupindukia unaweza kusababisha kuwa na mbegu zisizo na ubora hivyo kupata watoto inakuwa vigumu, hii ni kwa sababu mtu akinywa pombe damu inakuwa inachemka na kufanya joto kuongezeka. 

Dk. Mahenda anasema kwa kawaida korodani linatakiwa kupata joto pungufu ya digrii moja ya joto la kawaida la binadamu kama 35.2 hadi 36.2; ikizidi zaidi ya hapo huleta madhara. 

Wanaume wengi wakiwa na tatizo la nguvu za kiume hukimbilia haraka kutafuta dawa badala ya chanzo cha tatizo hilo. 

Hali hiyo imesababisha wengine kupata madhara zaidi sehemu zingine za mwili kutokana na dawa hizo kutothibitishwa kisheria. 

“Wanaume wengi wanamatatizo ya uzazi lakini hawataki kuja hospitali wanawake ndio wanahangaika, nawashauri wanaume wajitokeze kupima nguvu za kiume na si kutumia dawa hovyo. 

“Kila anayejihisi tujue tatizo liko wapi tumpatie tiba anayostahili na utakuta wakati mwingine tiba yake wala sio dawa mfano, mgonjwa wa sonona huwa tunampatia ushauri wa kusamehe halafu anarudi kwenye hali yake ya kawaida. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles