24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ummy awapa neno bodi ya mashirika yasiyo ya kiserikali

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezindua bodi ya nne ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, huku akiitwisha mambo manne ikiwemo kufuata sheria, kanuni na taratibu katika maamuzi yao.

Machi 27 mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alimteua Dk. Richard Sambaiga kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo.

Akizungumza jana jijini hapa wakati wa uzinduzi huo, Waziri Ummy alisema Serikali kwa sasa haitaiingilia bodi hiyo katika utendaji kazi wake ila akaitaka kusimamia sheria, kanuni katika maamuzi yao.

“Sasa hivi kila kitu mtafanya nyinyi, sisi hatuwezi kuwaingilia, ila maamuzi mtakayofanya ni lazima yawe ni kwa ajili ya manufaa ya nchi, simamieni sheria, kanuni na taratibu,” alisema Waziri Ummy.

Pia aliitaka bodi hiyo kuwa wawazi katika utendaji kazi wao, kutenda haki pasipo kumkandamiza mtu na kujifunza uzoefu wenye manufaa kutoka kwa nchi nyingine.

“Lazima hili mliangalie, hawa wanaoomba hii miradi waache vitu vinavyoonekana mfano shule, madarasa, kuliko kusema tu, tunataka tuone vitu kwa vitendo, Watanzania wa leo wamekuwa tofauti, haiwezekani ipatikane zaidi ya Sh bilioni tatu halafu kuwe hakuna kitu chochote kinachoonekana,” alisema Waziri Ummy.

Aidha aliyataka mashirika hayo kupeleka miradi hadi katika maeneo ya vijijini tofauti na sasa ambapo wamejikita zaidi mijini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. John Jingu, alisema kwa sasa kuna mashirika yasiyokuwa ya kiserikali 8,310.

“Hii ni sekta muhimu sana na nimtoe wasiwasi mwenyekiti aliyepita kazi zao hazijapotea, zipo,” alisema Dk. Jingu.

Awali aliyekuwa Mwenyekiti wa tatu wa bodi hiyo, Rukia Masasi, alilalamika bodi hiyo kutengwa na Serikali huku akidai hawajawahi kukaa kikao zaidi ya miaka mitatu.

“Nashindwa nizungumze nini, ni miaka mitatu sijawahi kukaa kikao chochote na mtu yeyote, ninachoomba tukutanishwe na hii bodi mpya tuwape tuliyonayo kuliko tunavyofanya kazi sasa hivi kila mmoja kivyake,” alisema Masasi.

Naye, Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Dk. Richard Sambaiga, aliomba ushirikiano kutoka kwa bodi iliyopita pamoja na serikalini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles