29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Mfumo wa stempu waongezea mapato TRA

Na KOKU DAVID

-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 42.8 zilizotokana na makusanyo ya ushuru wa bidhaa kupitia mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere alisema makusanyo hayo yametokana na ushuru wa bidhaa uliokusanywa katika kipindi cha mwezi Machi 2019.

Kichere alisema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la Sh bilioni 3.5 ambazo ukuaji wake ni asilimia 9 ukilinganisha na kipindi kama hicho ambacho kabla ya matumizi ya mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki walikusanya Sh bilioni 39.3.

Alisema mfumo huo ambao kwa awamu ya kwanza ulianza kutumika Januari 15, mwaka huu ulihusisha bidhaa za sigara, pombe kali, mvinyo, bia na aina zote za vileo.

“Katika awamu ya pili itakayoanza mwezi Mei itahusisha bidhaa za vinywaji baridi, maji, juisi pamoja na CD/DVD na kwamba hadi sasa tumeshafunga mitambo 44 katika viwanda 23 vya bidhaa za awamu ya kwanza.

“Pia tumefunga mitambo hiyo katika viwanda vyote vya sigara nchini ambavyo vipo vinne, viwanda vyote saba nchini vya bia, viwanda vya mvinyo na pombe kali ambavyo vipo 12 ikiwa ni pamoja na viwanda vidogo saba ambavyo vinatumia mfumo huu kwa kubandika stempu hizo kwa mikono chini ya uangalizi wa TRA kutokana na uchanga wa teknolojia ya mitambo yao ya uzalishaji,” alisema.

Kichere alisema katika ufungwaji wa mfumo huo kwa viwanda vya bidhaa za awamu ya pili wameshafunga mitambo 45 katika viwanda 19 vya vinywaji baridi.

Alisema matumizi ya mfumo huo wa stempu za kodi za kielektroniki yamekuwa na faida na kwamba yamewezesha kuongeza mapato kutokana na ushuru wa bidhaa, kuondoa malalamiko ya kutokutendewa haki katika makadirio ya kodi, Serikali kutambua mapema ushuru wa bidhaa utakaolipwa.

Aidha, alisema faida nyingine ni kuzibwa kwa mianya ya uingizaji nchini wa bidhaa kiholela ambazo hazijalipiwa ushuru stahiki na zisizokuwa na viwango vinavyokubalika, kuongeza uhiyari wa kulipa kodi, kuwezesha ufuatiliaji wa bidhaa pamoja na kulinda afya ya mlaji kwa kumwezesha mtumiaji au msambazaji kutambua bidhaa yenye stempu halali na isiyo halali.

Kichere alisema matumizi ya stempu za kodi za karatasi yalikuwa na changamoto ambazo zilisababisha upotevu wa mapato ya Serikali, uwezekano mdogo wa kutambua stempu za kughushi, kuibuka kwa wadanganyifu waliotumia udhaifu wa mfumo wa stempu za karatasi kwa kuiibia Serikali kwa kughushi stempu.

Aliongeza kuwa kwa matumizi ya stempu za kodi za karatasi haikuwa rahisi kutambua uhalali wa bidhaa iliyokuwa sokoni kuwa imetengenezwa na mzalishaji halali wa bidhaa hiyo.

“Matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki yalianzishwa mwaka 2018 na Serikali kupitia mamlaka ya mapato kwa bidhaa zinazostahili kutozwa ushuru wa bidhaa ili ziweze kutozwa kwa mujibu wa kifungu namba 124 cha sheria ya ushuru wa bidhaa sura ya 147 inayoainisha aina za bidhaa zinazotozwa ushuru huo kwa mujibu wa jedwali namba 4 la sheria hii,” alisema Kichere.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles