MATUKIO ya ulawiti na ubakaji kwa watoto mkoani Kilimanjaro, yametajwa kuongezeka kutokana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Hayo yameelezwa jana na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alipokuwa akizungumza na wananchi katika semina maalumu ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo.
Semina hiyo ilifanyika katika Kata ya Pasua, mjini Moshi mkoani hapa.
“Vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo hasa wanafunzi wa shule za msingi katika maeneo mbalimbali mkoani hapa, yamezidi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ushirikina na ukosefu wa malezi bora kutoka kwa wazazi na walezi.
“Suala hili linasababishwa na wazazi na walezi kuwa ‘bize’ na utafutaji wa pesa kuliko malezi ya watoto wao.
“Ili kukabiliana na tatizo hili, lazima wazazi na walezi mbadilike kwani tunakoelekea si pazuri,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, katika Manispaa ya Moshi pekee, matukio ya ubakaji yaliyoripotiwa ni zaidi ya 102 na matukio ya ulawiti ni 33.
“Katika matukio hayo ya ubakaji wa watoto, wapo walioathirika moja kwa moja kwa kupewa ujauzito kwani waliobebeshwa mimba ni 31.
“Wengine walilazimika kukatisha masomo yao, jambo ambalo ni la hatari na linajenga kizazi kibaya,” alisema.
Aliyataja makundi yanayoongoza kwa kufanyiwa ukatili huo kuwa ni watoto wa kike wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 13.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari, Anna Mkapa iliyopo katika kata hiyo, Patrick Madili, alisema tabia ya wazazi kuwapa watoto wao simu za kisasa imechangia kwa kiasi kikubwa kuathiri nidhamu za wanafunzi.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao ili wasiharibikiwe kimaadili.