Nora Damian -Dar es salaam
UJENZI wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha kwanza kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro, umefikia asilimia 87 huku Sh trilioni 1.7 zikiwa zimeshalipwa hadi sasa.
Kipande hicho cha kilomita 300 kilianza kujengwa Mei 2, 2017 na hadi kukamilika kwake kitagharimu zaidi ya Sh trilioni 2.
Akizungumza jana wakati Baraza la Uongozi wa Chuo cha Taifa Usafirishaji (NIT) lilipotembelea mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRC), Masanja Kadogosa, alisema uwekaji matuta umefikia asilimia 91 wakati madaraja na makaravati yakiwa yamefikia asilimia 90.
Alisema ujenzi wa stesheni ya Soga umefikia asilimia 100, Pugu (99), Ruvu (95), Ngerengere (93), Morogoro (90) na Dar es Salaam (85).
“Hali ya hewa na ardhi ndiyo changamoto kubwa zinazotusumbua katika mradi huu, kuna wakati ujenzi ulisimama kwa muda kwa sababu mvua zilikuwa kubwa sana, lakini hivi sasa kazi inaendelea vizuri,” alisema Kadogosa.
Kuhusu ziara hiyo ya NIT, alisema ina umuhimu mkubwa kwani bila kuwa na rasilimali watu ya kutosha miradi mingi inayoendelea sasa inaweza kushindwa kuendelezwa.
“NIT ni watu muhimu sana kwetu kwa sababu wafanyakazi wengi tulionao wamepitia katika chuo hiki, ‘human resource’ ni muhimu kwa sababu Serikali inapowekeza matrilioni kwenye miradi mikubwa kama hatuna watu wa kuiendeleza tutarudi kule kule,” alisema.
Katika kipande hicho cha Dar es Salaam – Morogoro, mbali ya kazi ya kutandika reli nyingine zinazoendelea ni ujenzi wa madaraja, makaravati, miundombinu ya ishara ya mawasiliano, nguzo za umeme na mahandaki.
Msimamizi wa ujenzi wa mahandaki katika eneo la Kilosa, Injinia Amir Hamis, alisema kazi inaendelea kwa kasi na kwamba mahandaki yote manne yako katika hatua za mwisho za ujenzi.
“Handaki la kwanza limefikia zaidi ya asilimia 98 na tunachomalizia sasa ni njia za watembea kwa miguu na kupitisha umeme. La tatu limemalizika kwa asilimia 100 sehemu ya juu na sasa tunaendelea na sehemu ya chini,” alisema Injinia Hamis.
Kwa upande wake Mkuu wa NIT, Profesa Zacharia Mganilwa, alisema ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujifunza na kuangalia namna wanavyoweza kuandaa rasilimali watu kwa sekta muhimu kama ya reli.
“Hatuna wataalam wa kutosha hivyo wakizalishwa kwa wingi hata wakandarasi wa Kitanzania kuwaajiri Watanzania wenye sifa na wakati mwingine tunaweza tusiwe na haja ya kuwa na wakandarasi wa nje,” alisema Profesa Mganilwa.
Alisema pia tayari wameandaa mitaala mipya ambayo itahusisha teknolojia za ujenzi wa reli ikiwemo ujenzi wa madaraja na mahandaki ili kujenga uwezo wa wataalam wa ndani.
“Mikoa yote ya Tanzania Bara imeshaunganishwa kwa reli na kinachofuata sasa ni kuunganisha kwa reli hivyo, lazima tujenge uwezo wa sisi wenyewe Watanzania kwa sababu hili ni taifa linaloendelea,” alisema.