25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Uingereza yajitayarisha kwa fujo

PINDI Uingereza itajitoa kutoka Umoja wa Ulaya hapo Machi 29, mwaka huu bila ya kuwapo mapatano baina ya pande hizo mbili, basi nchi hiyo itauimarisha sana mpaka wa Ireland ya Kaskazini (ambayo ni sehemu ya Umoja wa Ufalme wa Uingereza (United Kingdom) na Jamhuri ya Ireland (iliyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya).

Gazeti la Uingereza la Guardian limeripoti kwamba hadi polisi 1000 itabidi wapatiwe mafunzo maalumU ili wawekwe mpakani. Msemaji wa Baraza la Wakuu wa Polisi (NPCC) alihakikisha kwamba yako matayarisho ya aina hiyo, lakini hajataja idadi ya polisi watakaoshiriki.

Gazeti hilo lilisema polisi hao watatokea England, Scotland na Wales ili kuzuia fujo zozote zitakazotokea. Mafunzo hayo ni muhimu kwa vile vifaa na mikakati inayotumiwa Ireland ya Kaskazini inatofautiana na ile inayotumiwa katika sehemu nyingine za Umoja wa Ufalme wa Uingereza (United Kingdom).

Msemaji huyo anasema hali tofauti ya mambo inaweza ikatokea, ikiwa ni pamoja na michafuko na pia haja ya kuulinda mpaka. Alizikanusha habari zinazosema kwamba polisi wa Ireland ya Kaskazini tayari wameshaomba msaada.

Pindi mpaka wa kijani baina ya Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya Ireland utadhibitiwa (watu na bidhaa kukaguliwa kinyume na ilivyo hivi sasa) kuna hofu ya kutokea fujo miongoni mwa raia na kuchomoza vitendo vya kigaidi kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 1998.

Nafasi ya kukubaliwa mwafaka uliofikiwa hadi sasa  baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya ni ndogo. Desemba mwaka jana serikali ya London ya waziri mkuu Theresa May iliahirisha hadi katikati ya Januari hii kuuwasilisha bungeni muswada wa muwafaka huo ikihofiwa kwamba hautopata kibali cha wabunge wengi. Inatarajiwa kwamba hata hapo baadaye wabunge wengi bado wataendelea kuupinga.

Hali hiyo huenda ikasababisha Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya bila ya kuwapo mapatano yoyote hadi hapo Machi 29, mwaka huu. Kutoka siku hiyo maelfu ya kanuni na sheria zinazohusu biashara na usafiri unaovuka mipaka baina ya Uingereza na nchi 27 zilizobaki za Umoja wa Ulaya zitakoma kufanya kazi.

Kwa hivyo, usafiri wa watu na bidhaa mipakani utakaguliwa. Miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya, Jamhuri ya Ireland ndiyo hasa itakayopata hasara kubwa pindi Bunge la Uingereza litaukataa Muswada wa mapatano uliofikiwa baina ya Serikali ya London na Umoja wa Ulaya. Uingereza ndiyo soko muhimu kwa bidhaa za vyakula kutokea Ireland

Waziri wa kilimo wa Ireland, Michael Creed, alisema suala hilo linahusu mamia kwa mamilioni ya Euro ambayo Ireland itapoteza pindi Uingereza itajitoa kwa njia isiyokuwa ya mpangilio kutoka Umoja wa Ulaya. Kwa hivyo, itabidi Ireland iombe ruzuku ya  ziada kutoka Umoja wa Ulaya kwa ajili ya mazao yake ya kilimo.

Pindi Uingereza itajitoa kutoka Umoja wa Ulaya bila ya kuwapo mwafaka, yawezekana mazao ya Ireland yakatozwa ushuru mkubwa yanapoingia Uingereza. Wakati huo huo, Waziri wa Uingereza anayeshughulikia mashauriano juu ya nchi yake kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya, Stephen Barclay, ameonya juu ya uwezekano wa kuitishwa kura nyingine ya maoni ya wananchi wakiulizwa tena kama nchi hiyo ibakie ndani ya Ulaya au ijitoe.

Alisema: Kura ya pili ya maoni italeta mgawanyiko mkubwa zaidi. Mgawanyiko wa sasa katika Uingereza utakuwa mdogo ukilinganisha na mvutano utakaosababishwa na kura ya pili ya maoni. Taifa letu litapasuka zaidi, alisema Barclay.

Kutokana na wakati ulivyo, kura ya pili ya maoni haitowezekana kwa vile kutafanyika Uchaguzi wa Bunge la Ulaya mwisho wa Mei. Kabla ya Uchaguzi wa Bunge la Ulaya, haiwezekani kufanyika kura ya maoni. Nchini Uingereza ni lazima Uchaguzi wa Bunge la Ulaya ufanyike. Hiyo itamaanisha uchafuzi mkubwa wa demokrasia kwa vile raia hao hao waliopiga kura kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya mwishoni mwa Mei watatakiwa tena kupiga kura kulichagua Bunge la Ulaya, alisema Barclay.

Ikiwa karibu miezi mitatu kabla ya Uingereza kujitoa kutoka Ulaya, kutokana na uchunguzi wa maoni ya raia, yaonesha Waingereza wengi sasa wanapendelea kubakia ndani ya Umoja huo.

Pindi kura ya maoni itapigwa, basi asilimia 46 ya raia wataamua kubakia na asilimia 39 watataka kutoka. Uchunguzi huo ulifanywa na Taasisi ya YouGov. Asilimia 15 iliyobaki ni watu ambao hawajashiriki katika uchunguzi huo, hawajaamua upande gani wanaelemea au walikataa kusema chochote.

Pindi wakiwekwa kando watu ambao hawajaamua upande gani wako na wale walioulizwa lakini hawakutoa maoni yao, basi yaonesha  asilimia 54 ya Waingereza sasa wanataka kubakia ndani ya Umoja wa Ulaya na asilimia 46 wanataka kutoka.  Katika kura ya maoni ya mwaka 2016 raia waliopendelea kubakia ndani ya Umoja wa Ulaya walikuwa asilimia 48 na waliotaka kutoka walifikia asilimia 52. Huu uchunguzi wa sasa unaonesha vipi Waingereza walivyogawika katika suala hili.

Waziri Mkuu Theresa May anakataa kuitishwa kura mpya ya maoni. Yeye anajaribu kufa na kupona kupata wingi bungeni ili mpango wake wa kujitoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya kwa njia ya mpangilio uungwe mkono. Lakini licha ya maonyo kutoka kwa wanaviwanda, wakuu wa mabenki na wakulima, wabunge wa Kiconservative wenye vichwa ngumu wanashikilia kutaka kuiongoza Uingereza iwe nje ya Ulaya, hata bila ya kuwapo mwafaka.

Bado May anahisi anayo nafasi ya kuwashawishi viongozi wa nchi za Ulaya walegeze kamba kwa masharti yaliyofikiwa, ili angalau kuwatuliza wabunge huko London waukubali mwafaka uliopatikana hadi sasa.

Katika suala hili, yaonesha Waingereza wamejitia wenyewe kitanzi na kufikia katika hali hii ngumu ya sasa ya kutojua hasa nini la kufanya na nini wanataka. Hata kuuahirisha uamuzi wa kujitoa kutoka Ulaya una shida zake, utamaanisha kwenda kinyume na uamuzi  huru wa  wananachi walioutoa mwaka 2016 uliotaka nchi yao ijitoe kutoka Umoja wa Ulaya bila ya atiati yoyote.

Kuna wachunguzi wa mambo wanaosema kwamba hata kama hapo Machi 29 kutazuka vurugu, hii haitokuwa kiroja na mara ya kwanza katika historia ya Uingereza iliyofanya makosa mengi katika uhai wake.

Wanautaja mfano wa Mashariki  ya Kati iliyojeruhiwa na kutokwa na damu nyingi hadi leo ikiwa ni matokeo ya mbegu za vurugu zilizopandwa na Uingereza kwa kuchora mipaka ovyo ovyo katika eneo hilo.

Na sasa kukiwapo hofu ya kutokea mzozo mpya katika Ireland ya Kaskazini, Uingereza hiyohiyo inajaribu kupeleka majeshi mapya katika mpaka wa Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya Ireland. Yaonesha kwa Uingereza, dola iliyozowea kuzivamia nchi nyingine, vita maisha ni vizuri kwake na kutumia majeshi ndio njia rahisi kwake. Ni ajabu!

Kuna hatari huko mbele, nayo ni uwezekano wa kuzuka vita vipya vya kienyeji huko Ireland. Wachunguzi wa mambo, hasa wa nchi za Ulaya Bara, wanasema hiyo inatokana na historia ya Waingereza wengi ambao bado wanashikilia mawazo ya Kiconservative, kuifikiria nchi yao bado ni dola kuu la kikoloni, mfano kushikilia kubakia Irelnd ya Kaskazini na pia Gibralter iliyo mbali kabisa na London, au Visiwa vya Falkland vilivyoko maelfu kwa maelfu ya maili kutoka London na vilivyoko karibu kabisa na Argentina huko Amerika ya Kusini.

Bado Waingereza wanaliita taifa lao Muungano wa Ufalme wa Uingereza, chini ya Malkia na ikitumia sarafu ya Pauni yenye sura ya Malkia huyo, tena bila kujali hisia za watu wa nchi nyingine. Hicho si kichekesho tu, lakini pia ni hatari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles