*Lengo ni kukuza uchumi na uwekezaji nchini
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha uhusiano wa kimataifa ili kuchochea uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.
“Mheshimiwa Rais ameniagiza niwaambie kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kuwapokea, kuwasikiliza na kushirikiana nanyi katika kuimarisha shughuli za uwekezaji na biashara nchini,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne Novemba 16, 2021) wakati akifungua kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema katika kipindi kifupi Mheshimiwa Rais Samia ameboresha mahusiano na nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kukuza uchumi.
Amesema Rais Samia ameongeza usimamizi wa sera za soko huria, sera za kiuchumi na kifedha zenye mwelekeo wa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Amesema kwa kipindi cha Machi hadi Agosti 2021, Tanzania imeongoza kwa kuvutia kiwango kikubwa zaidi cha uwekezaji kutoka nje kwa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kiwango cha uwekezaji kutoka nje kilifikia Dola za Marekani bilioni 2.9.
Majaliwa amesema licha ya janga la UVIKO19, Tanzania katika mwaka 2020 ilipokea uwekezaji kutoka nje wa Dola za Marekani bilioni moja.
“Hili limefanikiwa kutokana na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji,” amesema.
Akizungumzia kuhusu mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Uingereza, Waziri Mkuu amesema Uingereza imeendelea kuwa mshirika wa asili, wa kihistoria na wa muda mrefu wa kibiashara wa Tanzania.
Waziri Mkuu ametoa wito kwa mamlaka husika za pande mbili kushughulikia vikwazo vya kibiashara visivyokuwa vya kikodi ili kurahisisha shughuli za kibiashara na huduma kwenye jamii zetu bila kuathiri misingi ya ushindani.
“Uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6.5 kutoka mwaka 2016 hadi 2020 na hivyo, kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika,” amesema.
Ameongeza kuwa hivi karibuni Serikali imeendelea kushuhudia uwekezaji mkubwa kutoka kwa makampuni ya Uingereza ikiwemo miradi 956 kutoka Uingereza yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.5 imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania pamoja na mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero (Dola za Marekani milioni 238) na kupatikana kwa leseni ya uchimbaji wa madini ya nickel ya Kabanga
Waziri Mkuu amemshukuru, , Mwakilishi Maalumu wa Waziri Mkuu wa Uingereza wa masuala ya kibiashara Lord Walney kwa kuitangaza Tanzania kuwa sehemu sahihi kwa ajili ya uwekezaji na biashara hususan kwa makampuni kutoka Uingereza.
Naye, Mwakilishi Maalumu wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Lord Walney, amesema Uingereza itaendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo na uwekezaji nchini Tanzania na wataendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukuza uchumi na uwekezaji.
Kwa Upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Kitila Mkumbo, amesema Mkutano huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwani unalenga kuongeza kiwango cha usafirishaji wa bidhaa kutoka nchini Tanzania kwenda Uingereza ili kuweka usawa katika bidhaa zinazoingia na kuuzwa miongoni mwa Nchi hizo mbili.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Geoffrey Mwambe, amesema lengo la kongamano hilo ni kupokea mrejesho wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Uingereza kuhusu mazingira ya ufanyaji wa biashara pamoja na kuboresha maeneo ambayo yana changamoto katika uwekezaji na kwa pamoja kuwa na maadhimio ambayo yatatengeneza fursa za kukuza uchumi na usawa wa kibiashara kwa nchi zote.
Waziri Mwambe amesema, Wizara ya Uwekezaji itaendelea kuendesha makongamano ya uwekezaji na wadau wa Sekta Binafsi pamoja na nchi washirika katika kuhakikisha wanatengeneza fursa na mazingira bora ya uwekezaji kwa kusikiliza mawazo na changamoto zinazowakabili wawekezaji.
Naye, Waziri Wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, anayeshugulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrick Soraga, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Uingereza kuwekeza katika sera ya Uchumi wa Bluu ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetengeneza mazingira bora ya kiuwekezaji kwa wawekezaji hususan katika Sera ya Uchumi wa Bluu.
Waziri Mkuu alihitimisha kwa kuwashukuru Washiriki wote wa kongamano hilo na kuwahamasisha kuendelea kuwekeza nchini Tanzania kwani Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara kwa kutoa vivutio vya kisera na visivyo vya kisera sambamba na cheti cha uwekezaji mahiri. Hatua nyingine ni kuhakikisha huduma zote muhimu ikiwemo vibali, leseni na baadhi ya vivutio vinapatikana kwenye kituo cha huduma cha pamoja.