23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

DC aonya Mgambo wanaojihusisha na uhalifu

Na Allan Vicent, Tabora

MKUU wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Sauda Mtondoo amewataka vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Akiba (Mgambo) kutoyatumia kwa kufanya uhalifu, badala yake wayatumie kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.

Mtondoo amtoa kauli hiyo jana alipokuwa akifunga mafunzo hayo yaliyokuwa na jumla ya askari 43 wa kata ya Igunga katika uwanja wa barafu mjini hapa.

Alisema Jeshi la Akiba linaundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ambayo imeweka bayana kuendeleza jeshi la akiba kwa ajili ya usalama wa raia ikiwemo kuzuia uhalifu.

Alibainisha kuwa katika mafunzo hayo yaliyoendeshwa kuanzia Julai 1 hadi Novemba 11, 2021 walipewa elimu mbalimbali ikiwemo nidhamu, usalama wa raia, mbinu za kivita, kwata, ujanja wa porini, utimamu mwili, uchimbaji wa mahandaki, jinsi ya kujikinga na adui kwa kutumia singe ujasiriamali na jinsi ya kumtambua adui kabla hajakutambua.

Pia walipewa elimu juu ya rushwa kwa kuwa rushwa ni adui wa haki hivyo anaamini kuwa kila askari wa jeshi la akiba atapinga kwa nguvu zake zote vitendo vya rushwa mahala popote atakapokuwa.

Aidha alisema hategemei kusikia askari yeyote wa jeshi la akiba akijiingiza katika vitendo viovu nakuwataka wakashirikiane pamoja na wananchi katika maeneo yao ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unalindwa. 

Aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwatumia katika shughuli mbalimbali na pindi fursa za ajira zinapopatikana za ulinzi watapewa kipaumbele.

Awali katika risala yao iliyosomwa na MG Zawadi Maura walimwomba DC kuwapa kipaumbele kwenye ajira za makampuni binafsi kwa kuwa wanaofanya kazi hizo mara nyingi ni raia ambao hawana mafunzo yoyote ya kijeshi.

Baadhi ya askari wastaafu Lazaro Ngullo aliyekuwa Mkuu wa upelelezi wilayani humo na Hussein Omar aliyekuwa Mkuu wa Gereza la wilaya hiyo waliwataka askari hao kutumia vizuri mafunzo hayo kwa kuwa ajira zipo nje nje wakati wowote huku wakiwaomba kutojiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles