MOMBASA, KENYA
RAIS Uhuru Kenyatta, amekiri kushindwa kupata suluhu kuhusu mgomo wa madaktari ambao umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya mwezi moja sasa, akisema serikali ilijaribu kila iwezalo bila mafanikio.
Kauli yake hiyo ambayo ilikuwa sehemu ya hotuba yake ya kuukaribisha mwaka mpya imeibua shaka iwapo kweli suluhisho litaweza kupatikana.
“Wakenya wenzangu, ingawa tumewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto, Wakenya wengi wangali wanakufa kutokana na maradhi yanayoweza kuzuiwa na kutibiwa. Nimeowaona wagonjwa wakiteseka madaktari wanapogoma.
“Tumejitahidi kupata suluhisho na madaktari, lakini kuna mipaka ya kile serikali inachoweza kumudu,” alisema akiwa Ikulu ya Mombasa.
Madaktari wameendelea na mgomo wao wakisema kuwa lazima mkataba uliopitishwa mwaka 2013 wa kuboresha mishahara na mazingira ya kazi utekelezwe.
Hali hii imewaathiri Wakenya wengi ambao wamekuwa wakitafuta matibabu katika hospitali za umma.
Hata hivyo, Rais Uhuru aliwahimiza Wakenya wamchague tena ili aweze kukamilisha miradi iliyoanzishwa na Serikali yake.
“Tuna uchaguzi katika muda wa miezi michache ijayo na itakuwa heshima kubakia kuwa rais wenu kwa kipindi kingine. Sababu yangu ya kuwania ni kukamilisha kazi tuliyoanza na kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kuimarika duniani,” alisema katika hotuba yake.
Rais alijivunia rekodi yake akisema kuwa utawala wake umefanya mengi kushinda zilizotangulia.
“Wakenya wenzangu, ninajivunia rekodi ya utawala wangu, tumefaulu mengi kushinda serikali zilizotangulia, na zaidi kushinda nchi nyingine ambazo tuko katika kiwango kimoja,” alisema.
Pia aliongeza kuhusu juhudi zinazofanywa kukabiliana na ufisadi huku akitaja kuwa tayari amepokea ripoti kuhusiana na kashfa ya michezo ya Olimpiki ya Rio.
“Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaangalia faili hiyo kuamua ikiwa kuna ushahidi wa kuchukua hatua zaidi kwa viongozi wa wizara ya michezo. Tuliahidi uwajibikaji na kuna mtu ambaye lazima atawajibika,” alisema.