26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ufaransa inastahili lawama Jaribio la mapinduzi Gabon,

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM

ASUBUHI ya Jumatatu wiki hii kulitokea tukio ambalo, wafuatiliaji wa karibu wa Taifa hili dogo la Gabon lililopo Afrika Magharibi hawakulitarajia- jaribuo la kuhitimisha miaka zaidi ya 50 ya utawala wa familia ya Rais Ali Bongo, ambaye yu matibabuni kwa miezi mitatu sasa nchini Morocco.

Kikundi cha waasi kijiitacho Vuguvugu la Vijana Wazalendo Jeshini na katika Vikosi vya Usalama vya Gabon kilitangaza tukio hilo kikimlaumu Bongo kwa matatizo yanayoikumba nchi hiyo na kuwa hana uwezo wa kuongoza kwa mujibu wa katiba kutokana na kutojiweza kiafya.

Waasi hao walisema wanataka kusimika tawala za kidemokrasia na kwamba hotuba ya kukaribisha Mwaka Mpya aliyoitoa Bongo kupitia mkanda uliorekodiwa akiwa hospitali mwishoni mwa mwaka jana baada ya ukimya wa muda mrefu uliozua wasiwasi kuhusu uwezo wake wa kuendelea kuongoza kikatiba ilikuwa danganya toto.

Walisema mtiririko wa hotuba hiyo haukupangiliwa vyema na sauti yake ilikuwa dhaifu, kitu kilichodhihirisha kuwa afya yake si njema na hivyo kukosa sifa ya kuwa rais.

Waasi walikuwa wamefanikiwa kukishikilia kituo cha taifa cha redio kwa saa mbili na kukitumia kuutangazia umma mafanikio ya mpango wao huo na kutoa mwito kwa wananchi na askari hususani vijana kujitokeza kuungana nao katika harakati hizo.

Hata hivyo, katika kile kilichoonekana hawakuwa wamejipanga vyema, jaribio hilo lilizimwa kirahisi na askari watiifu kwa familia ya Bongo na hivyo Kiongozi wa waasi wa kijeshi, aliyeongoza jaribio hilo la mapinduzi alikamatwa siku hiyo hiyo huku makomando wake wawili wakiuawa na wengine wawili kushikiliwa.

Licha ya kutojipanga vyema kwa waasi hao, tukio hilo liliwashangaza wengi kutokana na imani kuwa jeshi lina uaminifu mkubwa kwa familia ya Bongo isitoshe mara ya mwisho mapinduzi yalitokea nchini humo mwaka 1960.

Kama ilivyo kwa watawala wengi wa kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika wenye dhamira za kutawala maisha, Bongo alihakikisha analiweka kiganjani jeshi. Moja ya mbinu ni uteuzi wa maofisa wengi wakuu ikiwamo kikosi muhimu zaidi cha ulinzi wa rais kutoka jimboni kwake.

Lakini pia kwa upande mwingine ujio wa jaribio hilo si wa ajabu kwa kuzingatia mwelekeo wa hivi karibuni wa kisiasa hasa baada ya uchaguzi wa 2016, ambao upinzani uliporwa ushindi.

Mbali ya nguvu mpya ya upinzani chini ya mwanasiasa na mwanadiplomasia mashuhuri duniani, Jean Ping, kitendo cha Bongo kuwa nje ya nchi hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu akipokea matibabu nchini Morocco kimemdhoofisha zaidi kikatiba.

Awali aliugua kile kinachoelezwa lakini pasipo kuthibitishwa rasmi kuwa maradhi ya kiharusi wakati akihudhuria mkutano mkubwa wa uchumi nchini Saudi Arabia Oktoba 24 mwaka jana na kulazwa katika Hospitali ya Mfalme Faisal kabla ya kuhamishiwa Morocco.

Kufuatia kutoonekana kwake nchini humo kwa kipindi kirefu hali ya wasiwasi ilizuka na mvutano wa kimamlaka kujitokeza.

Kuona hilo kama tutakavyoona katika aya zinazofuata, Serikali ikatafuta msaada wa Mahakama ili kuweka sawa maslahi ya Bongo, kwa maana ya kuhakikisha anabakia madarakani.

Hadi sasa hakuna tarehe rasmi iliyotangazwa kwa Rais Bongo kurejea nyumbani na msemaji wake, Ike Ngouoni alikaririwa na duru za habari akisema Kiongozi huyo amekuwa akisumbuliwa na kizunguzungu kikali lakini sasa afya yake inaimarika.

Novemba mwaka jana, Mahakama ya Katiba ya Gabon chini ya Rais wake, Marie-Madeleine Mborantsuo ilitangaza marekebisho madogo ya Katiba katika ibara inayozungumzia hatua za kuchukua iwapo Rais hatoweza kwa muda fulani kutekeleza majukumu yake.

Uamuzi huo wa mahakama ulikuja baada ya Makamu wa Rais Pierre-Claver Maganga Moussavou kuitaka iingilie kati ili kuondoa ombwe la uongozi nchini humo kwa kutumia ibara za 13 na 16 za Katiba.

Moussavou aliitaka Mahakama kutamka ni nani kwa mujibu wa Katiba anayepaswa kuongoza vikao vya baraza la mawaziri ili chombo hicho kiweze kushughulikia masuala muhimu ya taifa katika kipindi ambacho rais hatokuwepo kwa muda.

Kipengele kipya kilichoongezwa kwenye Katiba katika marekebisho yaliyotangazwa na mahakama kimetoa nafasi ya baadhi ya majukumu kutekelezwa na makamu wa rais au waziri mkuu na makamu wa rais amepewa nguvu ya kuitisha na kuongoza vikao vya baraza la mawaziri.

Mahakama ya Katiba imetetea uamuzi wake huo kwa kusema unalenga kuhakikisha shughuli za uendeshaji nchi hazikwami na huduma za umma zinaendelea bila kutatizwa.

Upinzani umeikosoa hatua hiyo kuwa ni jaribio la kuimarisha madaraka ya ukoo wa Rais Bongo. 

Mtaalamu wa masuala ya siasa nchini Gabon Andre Adjo amesema uamuzi wa mahakama umeunda masharti mapya ambayo hapo awali hayakuwepo kikatiba.

Kwa mujibu wa Adjo, Katiba ya Gabon kabla ya marekebisho hayo tayari ilikuwa imeweka masharti ya kuitishwa uchaguzi ndani ya siku 45 ikiwa rais atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa kujiuzulu, kifo au sababu za kiafya.

Kwa namna hiyo uamuzi binafsi wa mahakama wa kupitisha kipengele kipya hauweki ukomo wa ni muda gani rais aliyeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu za kiafya anapaswa kuachia madaraka na uchaguzi mpya kuitishwa.

Kwa kutazama maamuzi ya mahakama yameshirikiana na Serikali kuulinda ukoo huo, kuhakikisha hauondoshwi madarakani mara hii kwa matumaini kuwa Bongo atapona na kurudi ,madarakani bila kujali kwamba anayejua uzima wake ni Mungu pekee.

Baba yake Rais Ali Bongo, Omar Bongo aliiongoza Gabon tangu 1967 hadi alipofariki dunia mwaka 2009 akiwa madarakan. Familia hii imetuhumiwa kujilimbikizia mali na utajiri mkubwa unaotokana na rasilimali lukuki za taifa hilo.

Ali Bongo,alichaguliwa kuongoza baada ya kifo cha baba yake mwaka 2009 na mwaka 2016, alipata ushindi finyu kwenye uchaguzi uliokumbwa  ghasia, mauaji na tuhuma za wizi wa kura.

Kwa sababu hiyo, miaka ya karibuni imekuwa ikishuhudia machafuko na maandamano ya mara kwa mara yakichagizwa na nguvu kubwa iliyo nayo upinzani.

Yote yanayotokea katika taifa hili ingawa inaweza ‘isionekane hivi kwa macho ya kawaida’, Ufaransa kwa kiasi kikubwa inapaswa kubeba lawama.

Ufaransa, ambayo iliitawala Gabon kuanzia mwaka 1885 hadi ilipotoa uhuru kwa taifa hilo mwaka 1960, ikizungumzia jaribio hilo ilitoa kauli ya kulilaani vikali, ikisema harakati zozote za kubadili mamlaka kinyume na katiba hazikubaliki na si suluhu ya amani na utulivu.

“Utulivu wa Gabon unawezekana kwa kufuata Katiba,” msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Agnes von der Muhll alisema mjini  Paris, akitoa msimamo wa Ufaransa kupinga jaribio hilo.

Lakini Gabon ni moja ya mifano ya kuhuzunisha sana ya sera za zama za Vita Baridi ijulikanayo kama ‘Françafrique’ ambayo ilitoa mwongozo namna Ufaransa itakavyohusiana na makoloni yake ya zamani.

Sera hiyo hata hivyo ilitengeneza vibaraka, iliyowalinda na kuwaimarisha madaakani, yaani madikteta, ambao itawatumia kundelea kunufaika na maliasili, uwekaji wa kambi za kijeshi na kujenga na kulinda ushawishi wake unaopungua eneo hilo baada ya kutoa uhuru.

Katika kesi ya Gabon, utajiri wa madini hasa ya uranium ulikuwa sehemu ya mkakati wa Ufaransa.

Kutokana na mchango huo hasi wa Ufaransa, tangu uhuru wake kutoka taifa hilo la Ulaya, Gabon imeendeshwa kama himaya binafsi ya kifalme na utawala wa majizi na wala rushwa (kleptocracy) na familia moja tu: akina Bongo.

Utajiri wao — ambao uliohifadhiwa katika mabenki ng’ambo ikiwamo Paris, miliki za kifahari katika wilaya za kitajiri za mji huo mkuu wa Ufaransa na French Riviera-kitongoji cha matajiri kilichokusanya wasanii na wanamichezo nyota pamoja na watu wengine maarufu katika pwani ya kusini mashariki mwa Ufaransa, na katika magari ya kifahari—ni simulizi kubwa nchini humo kama ilivyo rushwa na ufisadi katika utawala huo.

Taifa hilo lina akiba kubwa ya mafuta, lakini watu wake wamebakia masikini sana na lina moja ya viwango vya juu kabisa vya idadi ya vifo vya watoto wachanga duniani.

Ali Bongo — rais ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2016 licha maandamano na migomo ya upinzani wakishinikiza kurudiwa kuhesabiwa upya kwa kura, alitangazwa mshindi katikati ya kelele za kupinga— ni mtoto wa Omar Bongo, ambaye alitawala nchi hiyo kwa miaka 42 kuanzia mwaka 1967 hadi kifo chake mwaka 2009.

Kabla ya chaguzi hizo, Jean Ping, mgombea urais wa upinzani na ambaye ni mwanadiplomasia mashuhuri duniani aliyemkabili Bongo, alionya kuwa nchi ingeingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe iwapo maendeleo ya demokrasia hayatafikiwa. Na aliilinganisha nchi hiyo na meli ya Titanic iliyozama miaka mingi iliyopita, ambayo ni simulizi hadi leo hii.’

 Ping, ambaye baba yake ni Mchina alisema alikuwa mshindi halali wa uchaguzi huo na kwamba waangalizi wa kimataifa kutoka Ulaya wanafahamu hilo fika.

Akiwa na umri wa miaka 73, Ping awali aliitumikia serikali ya familia hiyo kwa miaka 10 kabla ya kuteuliwa kutumikia mashirika mbalimbali ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika (AU) ikiwamo uenyekiti wa Tume ya AU.

Baba huyo wa watoto wanane, aliwahi kuwa mshirika wa Pascaline Bongo, binti wa Omar Bongo anayefahamika kwa matanuzi na maisha ya kujirusha na ambaye wana watoto wawili.

Licha ya hayo, ilionekana wazi katika taifa hilo mtu asiye na ubini wa Bongo achana na uhusiano nayo kifamilia hastahili wadhifa huo.

Tukirudi kwa Ufaransa, haifahamiki wazi iwapo Ufaransa bado inaidhibiti Gabon au kwa namna nyingine ile.

Lakini imekuwa ikivumishwa kwa miongo kadhaa kuwa akina Bongo wamekuwa wakifadhili wanasiasa wa Ufaransa.

Rais wa zamani wa Ufaransa, Valéry Giscard d’Estaing alidai kuwahi kuona ushahidi wa kiinteljensia kuwa Bongo alikuwa akimfadhili aliyekuwa mpinzani wake Jacques Chirac.

D’Estaing alisema alimshukia Bongo kwa njia ya simu na kulikuwa na ukimya mrefu, ambao anaukumbuka hadi leo. Mwishowe Bongo akasema, ‘Ah, kumbe unajua.;

Mwaka 2008, baada ya Bongo kumkosoa Waziri wa Ufaransa Jean-Marie Bockel kwa kumshambulia kuhusu ‘upotevu wa fedha za umma’, waziri huyo akafukuzwa kazi na Rais wa wakati huo Nicolas Sarkozy.

Madai ya wanasiasa wa Ufaransa kufadhiliwa na watawala wenye malengo binafsi wa Afrika si mapya, kwani uliokuwa utawala wa miongo zaidi ya minne wa Libya wa Muammar Gaddafi, nao unadaiwa kuwahi kuwasaidia wagombea urais wa Ufaransa akiwamo Sarkozy na wale wa Italia akiwamo Silvio Berlusconi.

Ikiwa Rais Bongo hatopona huo unaweza kuwa mwisho wa zama za utawala wa miongo mitano wa familia yake na utajiri mkubwa waliochuma wakiwa madarakani kwani sit u hakuonekani uwapo wa mrithi mwenye nguvu bali pia upinzani katu hautokubali hilo kutokea.

Ali Bongo ni nani?

Ali Bongo Ondimba alizaliwa Februari 9, 1959 mjini Brazzaville na alifahamika kama mwana wa Alain Bernard Bongo (baadae Omar Bongo Ondimba) na Josephin (baadae Patience Dabany).

Kumekuwa na mjadala iwapo Ali Bongo ni mwana wa Omar Bongo ikizingatiwa kuwa mama yake alikuwa mja mzito miezi 18 kabla ya kuolewa madai ambayo Ali Bongo amekuwa akipinga.

Baada ya kusomea uanasheria Ali Bongo alijitosa katika siasa za Gabon ambapo alijiunga na chama PDG mwaka 1981 na muda mfupi baadae aliteuliwa katika kamati kuu ya chama  Machi 1983.

Baadae aliteuliwa kumwakilisha baba yake katika chama hicho nafasi ambayo ilimwezesha kujiunga na asasi kuu ya uongozi wa chama katika uamuzi ambao ulifikiwa katika kongamano maalum ya PDG mwaka 1986.

Wakati wa utawala wa baba yake Ali Bongo aliwahi kuhudumu kama waziri wa mambo ya nje kati ya mwaka 1989 na 1991; pia aliwahi kuhudumu kama naibu kiongozi wa Bunge la Taifa kuanzia mwaka 1991 hadi 1999.

Wakati wa uchaguzi wa uraisi wa mwaka 2005 alifanya kazi kama mshirikishi wa vijana katika kampeini ya baba yake.

Baada ya uchaguzi huo alipandishwa cheo na kuwa waziri wa mambo ya nje wa Gabon kuanzia Januari 21 2006 huku akiendelea kushikilia wadhifa wa waziri wa ulinzi. Alishikilia wadhifa huo hadi mwaka 2009.

Ali Bongo alitarajiwa kuwa mrithi wa baba yake Omar Bongo ikizingatiwa kuwa alimteua katika nyadhifa muhimu katika utawala wake.

Hata hivyo, uungwaji mkono wa Ali Bongo ndani ya uongozi wa PDG ulihojiwa na vyombo vya habari na kulikuwa na maoni kwamba raia wengi wa Gabon walimchukulia kama ‘mtoto aliyedekezwa na kwamba hawezi kuwasiliana kwa lugha asilia ya nyumbani kwasababu alizaliwa Congo-Brazzaville, kulelewa Ufaransa.

Kufuatia kifo cha Baba yake aliyekuwa madarakani kwa miaka 41, alichaguliwa kuendelea na uongozi wa taifa hilo  Agosti 2009.

Siku chache baada ya uchaguzi uliyofanyika Agosti 30,  2009 alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata asilimia 42ya kura, matokeo ambayo yaliidhinishwa mara moja na Mahakama ya Katiba. Hatua, ambayo ilisababisha maandamano makubwa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Gabon.

Aliapishwa kuwa Rais, Oktoba 16 katika hafla iliyohudhuriwa na marais kadhaa wa mataifa ya Afrika. Rais Ali Bongo ana mke na watoto wanne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles